Mratibu wa Idara ya Jinsia wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Bi. Lupi Mwaisaka (katikati) akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Septemba 13, 2022 Jijini Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Bw. Ernest Kimaya akiongea na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 13, 2022 katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) ukiangazia mchango wa CHAVITA katika mapambano dhidi ya Uviko-19 hususan kwa viziwi na maandalizi kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Viziwi kitaifa mwaka huu.Mwanasheria wa masuala ya watu wenye ulemavu, Bw. Novath Rukwago akiongea katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) jijini Dar es Salaam leo Septemba 13, 2022 uliongazia mafaniko ya CHAVITA katika mapambano dhidi ya Uviko-19 hususan kwa viziwi na maandalizi kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Viziwi kitaifa.
**************************
Chama Cha Viziwi Tanzania kimetajwa kuwa msaada mkubwa katika kuwasaidia viziwi kote nchini katika jitihada za kuwafanya wafikie malengo mahususi waliyoijiwekea, kupata huduma stahiki na waweze kuishi sawa na jamii ya viziwi wengine kote nchini.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Septemba 13, 2022 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA), Bw. Ernest Kimaya kwenye mkutano ulioandaliwa na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) ukiangazia mchango wa CHAVITA katika mapambano dhidi ya Uviko-19 hususan kwa viziwa na ujio wa maadhimisho ya Wiki ya Viziwi kitaifa mwaka huu.
Bw. Kimaya amesema, wakati wa janga la ugonjwa wa UVIKO-19, pamoja na makundi mengine, watu wenye ulemavu walikuwa ni miongoni mwa wahanga wakubwa kwani shughuli zao za kila siku zilikuwa zinawahitaji wasaidizi na hivyo kuwafanya kuwa hatarini.
Kufuatia hilo, Kimaya ameendelea kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwani bado haujaisha ingawa kwa sasa kwa kiasi kikubwa umepungua nchini.
Kando na hayo, Kimaya amewataka wananchi wote kote nchini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Wiki ya Viziwi yatakayoanza Septemba 26 na kilele chake kitakuwa Oktoba Mosi na kitaifa maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Mtwara.
Kwa upande wake, Mratibu wa Idara ya Jinsia wa CHAVITA Bi. Lupi Mwaisaka amesema, CHAVITA pamoja na mambo mengine inafanya kazi ya kuondoa vikwazo vya mawasiliano kwa viziwi na kupata habari lengo ni kuleta maendeleo.
“CHAVITA inafanya kazi ya kuondoa vikwazo vya mawasiliano na kupata habari kwa viziwi lakini pia CHAVITA inafanya kila njia ya kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo” alisema Bi. Mwaisaka.
Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, Bi. Maswanya amesema
“Janga la ugonjwa wa UVIKO-19 ni lenye kushtusha na kushangaza, na kwa upande wetu sisi watu wenye viziwi tulikuwa nyuma sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, kumekuwa na habari, uelimishaji mafunzo na elimu iliyokuwa ikitolewa na vyombo vya habari na sehemu mbalimbali lakini kwa jamii ya viziwi ilikuwa yakiwapitia mbali”
Bi. Mwaisaka ameongeza kuwa, wao kama CHAVITA kupitia ufadhili wa wadau wao ambao ni shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto na wanawake katika mataifa yanayoendelea (UNICEF) wameweza kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na kuhamasisha kuchanja na kutoa elimu namna ya chanjo ya Uviko-19 inavyofanya na katika mikoa mitatu ya Arusha, Mbeya na Mwanza.
Katika mikoa hiyo, makundi mbalimbali yalifikiwa ikiwemo wanafunzi viziwi, wasio na viziwi, walimu na jamii ya watu wanaoishi katika mikoa hiyo ambapo zoezi la uhamishaji lilienda sambamba na kupatiwa chanjo kwa waliokuwa tayari huku mtazamo hasi dhidi ya chanjo za ugonjwa wa UVIKO-19 ukiondoka miongoni mwa jamii zilizofikiwa.
Naye mwanasheria wa masuala ya watu wenye ulemavu, Novath Rukwago akizungumza katika mkutano huo amesema, huduma stahiki na zenye viwango kwa watu wenye ulemavu ikiwemo viziwi ni jambo la lazima kwani lipo kisheria na ni mwongozo kupitia mikataba mbalimbali ya kimataifa hususan mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu.
Bw. Rukwago ameendelea kwa kusema kuwa, haki wanazopaswa kupatiwa kila mtu ikiwemo kupata habari ni muhimu kwa makundi yote ikiwemo viziwi hivyo hawapaswi kuwekwa kando hivyo ni jukumu la serikali katika kuhakikisha kwamba inaweka miundombinu wezeshi na mifumo rafiki ili viziwi waweze kupata huduma ya habari na mawasiliano.
Kufuatia hayo, Bw. Rukwago akatoa rai kwa serikali kwamba, taasisi zote zinazotoa huduma ya kimaongezi na vipindi vyote vinavyotoa elimu kwa umma vinapaswa kuwa na wakalimani wa lugha za alama.
Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) ni moja ya chama cha kitaifa cha watu wenye ulemavu kwa upande wa viziwi chenye malengo ya kuleta msukumo wa maendeleo ya viziwi nchini katika nyanja mbalimbali na kuhakikisha kwamba viziwi kote nchini wanapata haki zao za msingi kama wananchi wengine kwa kuondoa vikwazo vya mawasiliano ambavyo vinawakumba kwa kushirikiana na wadau, serikali, wazazi /walezi na watu binafsi