************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amewataka wakazi wa Kijiji cha Kilombero Wilayani Simanjiro kuvuta subira juu ya sakata la kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho Nguti Kilusu.
Mwenyekiti huyo amesimamishwa uongozi wake na kamati ya siasa ya CCM wilaya ya Simanjiro kwa tuhuma ya kuuza kinyemela eneo la ardhi ya kijiji hicho kwa baadhi ya wafanyabiashara wa jiji la Arusha.
Makongoro akizungumza na wananchi wa kijiji hicho amedai kuwa anarudisha sakata hilo likajadiliwe upya na CCM, chama kilichomdhamini ili agombee nafasi hiyo kwani hakikumfutia uanachama ila kilimsimamisha uongozi wake.
Amesema hatua tatu za kuondolewa kwa Mwenyekiti huyo wa kijiji hazikufuatwa hivyo hawezi kutoa maamuzi yake hadi hapo kamati ya siasa ya wilaya iliyomsimamisha itakapotoa upya uamizi huo.
“Hatua tatu zinazopaswa kufuatwa kwa ajili ya kuondolewa kwa Mwenyekiti huyo hazikufuatwa hivyo nalirudisha sakata hilo kwa kamati hiyo ya siasa ambayo mkuu wa wiilaya ni kamisaa na mjumbe ili lijadiliwe upya,” amesema Makongoro.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amewataka wananchi wa eneo hilo kuuungana pamoja na kusamehe ya nyuma ili wasonge mbele kwa ajili ya maendeleo.
Diwani wa Kata ya Shambarai, Julius Mamasita amepongeza hatua hiyo kwani CCM iliona mapungufu ya Mwenyekiti huyo katika uuzaji wa ardhi na kuchukua uamuzi wa kumsimamisha.
Mkazi wa kijiji hicho Michael Kilusu amesema Mwenyekiti huyo amesimamishwa kihalali kwani ameshiriki kuuza ardhi ya eneo lililotengwa kwa ajili ya mifugo hivyo kuzua mgogoro.
Mkazi wa kijiji hicho Maria Christopher amesema siasa chafu zimetumika kumuondoa Mwenyekiti huyo na kusababisha shughuli za maendeleo kusimama.
Hata hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti huyo Nguti Kilusuu amesema hatua hiyo ni nzuri kwani haki itapatikana na maamuzi mazuri yatatolewa upya.