*********************
Mteule, SACP. Mzee Ramadhani Nyamka, alizaliwa mwaka 1964 Mkoani Tanga, Wilaya ya Tanga Mjini na alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Muhimbili mwaka 1973 hadi 1979, na alihitimu elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari Mzizima, D’Salaam mwaka 1983.
Oktoba, 1995 kabla ya kujiunga na Jeshi la Magereza alihamia Makao Makuu ya Magereza akitokea Wizara ya Fedha akiwa Mtumishi Raia. Aidha, Januari mosi, 1996 alijiunga rasmi na Jeshi la Magereza ambapo alihudhuria mafunzo ya Uongozi daraja la kwanza na kuhitimu mafunzo hayo Mei 31, 1996 katika Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga.
Mwaka 1995 alipata Stashahada ya Juu ya Uhasibu katika Chuo cha IFM D’Salaam. Aidha, mwaka 2004 alitunukiwa Stashahada ya Uzamili ya Uhasibu katika Chuo cha IFM D’Salaam.
Katika Utumishi wake ndani ya Jeshi la Magereza amepandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo:- Mkaguzi Msaidizi wa Magereza (1996 hadi 2001), Mkaguzi wa Magereza (2001 hadi 2005), Mrakibu Msaidizi wa Magereza (2005 hadi 2009), Mrakibu wa Magereza (2009 hadi 2011), Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (2011 hadi 2013), Kamishna Msaidizi wa Magereza (2013 hadi 2017), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (2017 hadi anapata uteuzi wa CGP).
Aidha, Mteule CGP Nyamka ni mbobezi katika Tasnia ya masuala ya kifedha kwani amehudhuria mafunzo mbalimbali ya fani hiyo ikiwemo Mafunzo ya Uhasibu wa Sekta za Umma, Mafunzo ya Mifumo Jumuishi ya Usimamizi wa Fedha na mafunzo ya kugundua na kuzuia udanganyifu (Fraud Detection and Prevention).
Amewahi kufanya kazi katika nafasi ya Mkufunzi katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) mwaka 2001 hadi 2005, Mhasibu wa Magereza Mkoa wa Iringa mwaka 2005 hadi 2009, Mkufunzi katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) mwaka 2009 hadi 2011, Mkuu wa Sehemu ya Hoja na Ufungaji Mahesabu mwaka 2012 hadi 2014, Afisa Mnadhimu Magereza Mkoani Pwani mwaka 2014 hadi 2015, Afisa Mnadhimu Magereza Mkoa Morogoro mwaka 2015 hadi 2017, Mkuu wa Magereza Mkoa Morogoro mwaka 2017 hadi 2018, Afisa Mnadhimu Jeshi la Magereza mwaka 2018 hadi 2021, Kaimu Kamishna Huduma za Urekebishaji Jeshi la Magereza mwaka 2021 hadi anapata uteuzi wa CGP.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato Dodoma.