Kamanda wa polisi mkoani Arusha Justine Masejo akionyesha magunia hayo ya bangi yaliyokamatwa mkoani Arusha.
***********************
Julieth Laizer, Arusha
Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamshikilia dereva wa lori aliyejulikana kwa jina la Allen Wilbard Kasamu (49) mkazi wa Suye Jijini Arusha akiwa anasafirisha madawa ya kulevya aina ya mirungi yenye uzito kilo 390.75.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Septemba 11, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo amesema kuwa September 10, 2022 muda wa saa 12:30 asubuhi eneo la Kikwe wilayani Arumeru, walimkamata Kasamu (49) akiwa anasafirisha madawa hayo kwa kutumia gari aina ya Mitsubish Canter – Tanker ambalo ni maalumu kwa ajili ya kubeba mafuta.
“Hili ni gari la kubeba mafuta lakini yeye alijaribu kufanya uhalifu wa kusafirisha madawa ili asijulikane lakini mwisho wa siku ameishia mikononi mwetu”
Kamanda Masejo alisema kuwa, dereva huyo Ni mmoja wa watuhumiwa 38 wanaoshikiliwa na jeshi hilo waliokamatwa katika matukio tofauti mkoani Arusha kwenye operation iliyofanyika kwa Siku tano kuanzia September tano Hadi 10 mwaka huu.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo walifanikiwa kukamata pikipiki 13 zilizokua zinatumika katika matukio ya uhalifu, gongo lita 8, bangi yenye uzito wa kilo 70 pamoja na laptop 03.
“Watuhumiwa wote bado tunawashikilia kwa upelelezi ikiwemo kuwahoji na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya kutolewa maamuzi” alisema kamanda Masejo
Kamanda Masejo ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao sambamba na kuiweka mkoa wa Arusha katika Hali ya usalama.
“Pia nitumie nafasi hii kuwaonya baadhi ya watu wanaojihusisha na uhalifu hususani biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani tutaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua”
Katika hatua nyingine Kamanda Masejo amesema kwa Mkoa wa Arusha wananchi wameanza kujitokeza kusalimisha silaha zao katika vituo vya polisi na kutoa rai kwa watu ambao wanamiliki silaha kinyume cha Sheria kufika katika vituo vya Polisi ama ofisi za watendaji wa mitaa kusalimisha silaha hizo katika kipindi hiki ambacho Serikali imetoa msamaha kwa ambao watasalimisha.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha wanaomiliki silaha kinyume na Sheria watumie vema fursa hii ya msamaha iliyotolewa kwani baada ya hapo jeshi letu litafanya msako mkali na watakaokutwa nazo Sheria itachukua mkondo wake dhidi yao”