*******************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WAZIRI wa Maendeleo wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Dkt.Dorothy Gwajima ametaja watoto waliobakwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 walikuwa watoto 5,899 sawa na wastani wa 491 kwa mwezi.
Aidha watoto waliolawitiwa ni 1,114 sawa na wastani wa matukio 93 kwa mwezi kwa kipindi hicho.
Akizungumza na viongozi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Pwani, Gwajima alisema asilimia 60 ya ukatili huo unafanyika majumbani kwenye familia alipo mtoto huku asilimia 40 ikifanyika mashuleni .
Alielezea, takwimu hiyo ni ya mwaka 2021/2022 kutoka Jeshi la polisi hazifurahishi na ni suala ambalo linapaswa kukomeshwa kwa nguvu kubwa .
Hata hivyo , Waziri huyo alielezea watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo kwa mwaka 2020/2021 ni watoto 27,369 kwa wastani wa matukio 1,140 kwa mwezi .
“Hii ni sehemu ndogo sana ya matukio yanayoripotiwa kwani mengi hayawekwi bayana ,Na wanaofanya ukatili huu ni watu wazima ,wote tunakubaliana ukatili ni adui wa maendeleo ya uchumi lazima tukomeshe suala hili.”alifafanua Gwajima.
Alieleza kwamba ,hivyo Serikali katika kupambana na kutokomeza ukatili wa kijinsia juhudi kubwa zinaendelea kufanyika zikiwemo kutekeleza mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022.