Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Makamu Mwenyekiti wa Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga Nabila Kisendi ameiomba jamii kutoa ushirikiano kwa viongozi wote wanaopinga ukatili ili kumaliza vitendo hivyo.
Ameyasema hayo leo kwenye kikao cha viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi za mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo kupanga mikakati ya kiutendaji inayoweza kufikia malengo yaliyokusudiwa na kampeni hiyo.
Madam Kisendi pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kuiomba jamii kutoa taarifa za ukatili ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi mbalimbali wa SMAUJATA katika kuibua na kuzuia vitendo vya ukatili kwenye jamii.
“Jamii iwe tayari kutoa ushirikiano kwa viongozi wa SMAUJATA kwa kuwa wakweli tuangalie ni vitu gani ambavyo vinatuzunguka kwenye jamii zetu ambazo si desturi na mila zetu mfano kwenye masuala ya kubakwa au kulawitiwa watoto kwahiyo tushirikiane na viongozi wa SMAUJATA kutoa taarifa kama kunaukatili ukitokea kwenye jamii yako unaweza kutoa taarifa kwenye namba 116 hii ni namba ambayo unapiga hata kama huna salio piga bure ili kutoa taarifa kwa wakati sehemu husika SMAUJATA tuko pamoja kupinga ukatili wa aina zote”. amesema Madam Kisendi
Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Nabila Kisendi amewaagiza viongozi wengine ngazi ya chini katika Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha wanaifikia jamii kwa kutoa elimu na kutatua kero za ukatili zilizopo.
“ Viongozi wanatakiwa kwenda kutoa elimu ya kupinga ukatili kwenye taasisi zote kuanzia mitaa, kata, wilaya mpaka Mkoa na vile vile kuzingatia malengo ya SMAUJATA na dira yake tunapoenda kutoa elimu tuhamasishe watu waitambue kampeni hii ya kupinga ukatili kwahiyo viongozi muwe makini sana kusimama kwenye malengo, dira na kanuni za SMAUJATA”. amesema Madam Kisendi
Aidha Madam Kisendi wakati akizungumza kwenye kikao hicho ameeleza dira ya SMAUJATA kuwa ni kutengeneza Taifa lenye kizazi huru chenye haki na usawa kitakachoweza kujitegemea kwa kuzitambua fursa na kutumia ujuzi, maarifa na vipaji katika kujenga jamii yenye maendeleo endelevu.
Amesema dhamira ya Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) ni kuwezesha na kuijengea jamii uwezo kwa kuitambua na kuiishi misingi ya haki na usawa huku akiwaagiza viongizi wa SMAUJATA ngazi ya wilaya kata na vijiji kufanya kazi kwa weledi, ushirikiana na kujituma kwa kila mmoja katika eneo lake.
Madam Kisendi ametaja malengo ya SMAUJATA kuwa ni pamoja na kuelimisha jamii kuondokana na fikra, Imani, Mila, Desturi na tamaduni zinazokinzana na maendeleo.
“Yapo malengo ya SMAUJATA ambayo viongozi wa Mkoa tunatakiwa kuyazingatia sana lengo la kwanza ni kushirikisha jamii katika kuainisha fursa na changamoto zinazoikabili, kushirikisha jamii katika kuiunganisha na kuiwezesha katika mchakato wa maendeleo ili kuinua ustawi wake lakini pia kuelimisha jamii kuondokana na fikra, Imani, Mila, Desturi na tamaduni zinazokinzana na maendeleo lingine ni kuwezesha jamii kutumia fursa ya sera za kisekta na mikakati yake katika kujiletea maendeleo”.
“Malengo mengine ni kutoa elimu kwa jamii kupitia semina, Sanaa, warsha, makongamano, vyombo vya habari, matembezi ya Amani, vipeperushi kuhusu haki, usawa, fursa na sera mbadala kwa maendeleo endelevu kuiwezesha jamii kutekeleza haki na malezi ya mototo pamoja na malengo mengine mengi tumambayo ni muhimu viongozi wa Mkoa wa Shinyanga tuyaelewe”. amesema Madam Kisendi
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga waliohudhuria katika kikao hicho wameahidi kwenda kushirikiana na jamii katika kupinga ukatili.
Viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga leo wamekaa kikao cha pamoja kwa kushirikiana na viongozi wa serikali Mkoa huo akiwemo Afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale pamoja na Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Shinyanga Ancila Katero ikiwa lengo ni kujadili mikakati na njia bora za kuibua vitendo vya ukatili.