……………………..
Na Eleuteri Mangi, WUSM
Tamasha la Tano la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Sanaa na Utamaduni (JAMAFEST) limefungwa rasmi Bujumbura nchini Burundi kwa Burundi kukabidhi Bendera ya Jumuiya hiyo kwa Sekretarieti hadi itakapotangazwa nchi ambayo itakuwa mwenyeji wa tamasha la sita.
Katika Tamasha hilo, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika Sanaa za Jukwaani ambapo Septemba 9, 2022 Muziki wa taarabu umepeperusha vyema bendera ya Taifa kupitia kikundi cha Taifa cha Taarabu Asilia kutoka Zanzibar huku wasanii nguli wa muziki huo Abdul Misambano na Mzee Yusufu wakiibua shangwe na nderemo kutoka kwa washiriki wa tamasha hilo pamoja na wananchi wa Burundi waliofurika katika viwanja vya Intwari jijini Bujumbura.
Akizungumzia ushiriki katika Tamasha hilo, Mratibu wa JAMAFEST Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Bi Leah Kihimbi amesema Tanzania imefanya vizuri kwa kuwaleta wasanii wengi kwa fani mbalimbali ikiwemo taarabu, muziki wa Singeli, ngoma za asili ikiwemo wanafunzi wa shule ya msingi Mwanyahina kutoka wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Sanaa za Ufundi za uchongaji, uchoraji, wasusi, wajasiriamali pamoja na watumishi wa Umma.
Akifunga tamasha hilo Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki, Vijana, Michezo na Utamaduni Burundi Bw. Severin Mbarubukeye amesema kuwa amefurahishwa kwa ushiriki wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye Tamasha la Tano JAMAFEST nchini humo.
Aidha, ameongeza kuwa linasaidia kuimarika umoja na mshikamano katika nchi wanachama kuwa sehemu moja kwa wakati mmoja kubadilishana na kujifunza uzoefu wa nchi wanachama kwenye masuala ya Utamaduni.
Tanzania katika tamasha la JAMAEFEST 2022 imewakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni Dkt. Emmanuel Temu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Dkt. Emmanuel Ishengoma, Mtatibu wa Programu ya Ukombozi wa Bara la Afrika Bw. Bonifance Kadili, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kilonzo Kiagho pamoja na watumishi kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Usaidizi wa Kijamii Eliabi Khalid Chodota kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, watumishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekniolojia, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wajasiriamali pamoja na wasanii wa muziki, ngoma za asili, wachoraji na wachongaji.