Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Wakili Amon Mpanju akifunga Mkutano wa Siku Mbili wa Wadau wa Ustawi wa Jamii, Kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Godwin Gondwe akizungumza na Wataalam wa Ustawi wa Jamii, walikuwa kwenye Kikao cha Siku mbili jijini humo, kujadili namna bora yakuwaondoa Watoto waishio Mitaani na kufanya kazi kilichofanyika jijini Dar Es Salaam.
Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona, akizungumza kwenye Mkutano wa Wadau wa Huduma za Ustawi wa Jamii ambapo Wajumbe walijadiliasuala yanayo wahusu Watoto waishio kwenye Mazingira Magumu na kufanya kazi.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo wa Siku mbili wakiwa wanakisikiliza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Wakili Amon Mpanju wakati wa kufunga Mkutano huo uliofanyika jijini Dar Es Salaam.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM)
…………………………………………….
Na WMJJWM, Dar Es Salaam
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amoni Mpanju, amewataka Maafisa Ustawi kote nchini, kujidhatiti katika utendaji wao na kushirikiana na watu wa kada zingine hususan viongozi wa dini na watu wenye ushawishi kwenye jamii wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Wakili Mpanju ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa Siku mbili uliofanyika jijini Dar es Salaama kuanzia tarehe 6-7 Septemba, 2022 na kuwaleta Wadau wa Ustawi wa Jamii kutoka kote nchini wakiwepo Maafisa Ustawi 26 kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara.
“Leo tunahitimisha Mkutano wetu wa Siku mbili, ambapo tumetoka na maazimio yasiyo pungua 12, ni rai yangu mkayasimamie haya kwakuwashirikisha viongozi wenu Makatibu Tawala muyawekee mpango kazi utakao leta tija na majibu kwa kile mtakacho kipanga kwani kada yenu ninyi ni muhimu katika kuifanya jamii kuwa na ustawi, lakini kashirikianeni na watu wengine kwenye maeneo yenu” alisema Wakili Mpanju.
Mapema wakati wa kikao hicho, iliibuliwa hoja ya baadhi ya Mabasi yanayobeba wanafunzi kutuhumiwa kuwafanyia vitendo vya kikatili watoto, ambapo sehemu ya maazimio imeonelea kwa wakati wa sasa ipo haja ya wamiliki wa Shule kuwekewa utaratibu wa kuajiri Makondakta wanawake (matroni).
Akiwa anachangia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe, alisema kutokana na visa vingi kuripotiwa kwenye Wilaya yake, wao wameazimia, kutunga Sheria ndogo ya kutaka kila gari la wanafunzi kuwa na kondakta Mwanamke (Matron) huku akiiomba suala hilo ikiwezekana lifanyike kwa nchi nzima.
Kwa Upande wake Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Baraka Makona, alisema kikao hicho cha Siku mbili kimewawezesha kutoka na Maazimio kadhaa ya kumkomboa Mtoto wa kitanzania kwani watoto ndio taifa la kesho.
Naye Mkaguzi wa Polisi kutoka Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mdadhiru Kato Makora amesema mambo yote yaliyotolewa kwao ni Maagizo hivyo akaahidi kuyasimamia kwakuzingatia maelekezo.
“Maazimio haya ambayo tumeyafikia hapa kwetu kama Jeshi la Polisi hii ni Amri ya Mamlaka hivyo lazima tukaitekeleze kwa maslahi mapana ya Ustawi wa Mtoto wa Kitanzania” alisema Makora.