**************
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa mashindano ya dunia ya utanashati, urembo na mtindo (Miss & Mister Deaf) kwa watu wenye matatizo ya kusikia ‘Viziwi’.
Mashindano hayo yanatarajia kufanyika Oktoba 23 hadi 31 mwaka huu katika Ukumbi wa Peacock Hoteli uliopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA), Habibu Mrope amesema mashindano hayo yatashirikisha washiriki 200 kutoka nchi mbalimbali.
“Mpaka sasa washiriki 160 wamejiandakisha kushiriki mashindano haya, hapa nchini tunawashiriki sita ambapo wavulana wawili na wasichana wanne,” alisema Mrope.
Aidha ameeleza Tanzania kuchaguliwa kuandaa mashindano hayo kutokana na amani, vivutio vya utalii, ukarimu na ushirikiano mzuri uliopo nchini.
“Tulichaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano kutokana na ukarimu mzuri tuliokuwa nao, pia vivutio vya utalii wetu kama Mlima Kilimanjaro.”
Mwenyekiti huyo aliwataja Miss & Mister Deaf ambao wataiwakilisha Taifa katika mashindano hayo ni Khadija Kanyama, Joyce Denis, Carlyone Mwakasaka, Durath Mwankis, Rajabu Ali na Russo Songoro.