Na Mwandishi Wetu,Kibiti
MWENYEKITI wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU),Tumaini Nyamhokya ameiomba Serikali kuangalia namna ya kusaidia kuondoa aina yeyote ya Makato ya Kodi ya tozo zinazoendelea kukatwa katika mishahara ya wafanyakazi .
Mwenyekiti huyo ambae ni Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania( TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema hayo kwenye Mkutano Mkuu wa kuwachagua viongozi wa Chama Cha wafanyakazi wa Serikali za mitaa tawi la Boma wilaya ya Kibiti.
Amesema TALGWU haipingani na hatua ya Serikali katika kutafuta mapato yake bali wanachoomba kutatuliwa ni namna wafanyakazi wanavyokatwa tozo katika mishahara yao na hivyo kukatwa mara mbili na kwamba hatua hiyo inamuumiza mfanyakazi .
Kwa upande wake Katibu Mkuu Chama Cha wafanyakazi wa Serikali za mitaa Taifa ( TALGWU) Mohamed Mtima amewataka viongozi waliochaguliwa kuhakikisha wanasimamia maslahi ya wafanyakazi.
Akizumgumza mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi la Boma Halmashauri ya Kibiti Ami Lipungandondo ameeleza watasimamia na kuwachukulia hatua kwa waajiri wanatakaokiuka kanuni ya uajiri.
Chama Cha wafanyakazi wa Serikali za mitaa kipo katika mchakato wa kuwapata viongozi wa matawi ya wafanyakazi katika Halmashauri za mkoa wa Pwani ambazo zimeanishwa kuwa na matawi ya TALGWU .