*************************
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) imeikabidhi Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) meli tatu zinazotoa huduma katika Ziwa Nyasa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuziweka meli hizo katika usimamizi madhubuti wa MSCL.
Meli hizo za MV. Njombe, MV. Ruvuma pamoja na MV. Mbeya II zilizogharimu Shilingi Bilioni 20.1 zimekuwa zikisuasua katika kutoa huduma kwa wananchi wa mwambao wa Ziwa Nyasa pamoja na nchi jirani kutokana na TPA kujikita zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya usimamizi wa bandari nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Uchukuzi Bi. Stella Katondo alisema kuwa TPA imekuwa ikisimamia meli hizo ili kuhakikisha wananchi wanaozunguka Ziwa Nyasa wanapata huduma ya usafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine lakini usimamizi wa meli ni jukumu la msingi la MSCL.
“MSCL imeanzishwa na Serikali kwa ajili ya usimamizi wa meli zinazomilikiwa na serikali nchini. Aidha, kwa kipindi kirefu sasa MSCL imekuwa ikisimamia meli za Serikali na kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Hivyo ni matarajio ya Serikali kwamba baada ya meli hizi kukabidhiwa kwa MSCL zitasimamiwa ipasavyo na kutoa huduma iliyokusudiwa,” Alisema.
Wakati akitoa taarifa ya meli hizo Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa alisema kuwa meli za mizigo za MV. Njombe pamoja na MV. Ruvuma zilianza kujengwa mwaka 2015 na kumalizika mwaka 2017 na kugharimu Shilingi Bilioni 5.5 kila moja huku zikiwa na uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja.
“Kwa upande wa meli ya MV Mbeya II ambayo ni meli ya abiria na mizigo, Mamlaka ya Usimamizia wa Bandari ilianza ujenzi wa meli hii mwaka 2017 kwa gharama ya shilingi bilioni 9.1 na ujenzi huo ulikamilika mwezi Oktoba,2020. Meli hii ilijengwa na Mkandarasi Songoro Marine na baada ya kukamilika ilianza kutoa huduma katika bandari za Ziwa Nyasa kupitia vituo 13 kuanzia bandari ya Kiwira hadi Mbamba bay na kurudi,” Alisema.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Nahodha Bembele Ng’wita aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuhamisha umiliki wa meli hizo kutoka kwa mamlaka iliyojenga kwenda kwa taasisi yenye uzoefu wa kuendesha meli hizo.
“Kama MSCL tunasema asante kwa hilo na kusaini hati ya makabidhiano ni ishara ya wazi kwamba sisi tumepokea kwa shukurani na tunaiahidi Serikali kwamba tutatekeleza majukumu yetu ya msingi, lakini pia tuwaahidi wananchi wanaotegemea huduma ya usafiri katika mwambao wa ziwa kuwa watapata huduma safi, salama, bora na kutoa ufanisi katika shughuli za usafirishaji,” Alisisitiza.
Akipaza sauti za wananchi katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano, Mbunge wa Jimbo la Kyela Mhe. Ally Mlaghila alisema kuwa wananchi hawajali taasisi inayosimamia meli hizo isipokuwa wanahitaji kupata huduma nzuri nay a uhakika.
“Tunachotegemea sasa ni kwamba MSCL mnaenda kututoa hapa tulipo kutupeleka hatua nyingine mbele, tumieni masoko yaliyopo, tunaomba msiache soko la Malawi, endelezeni walipoishia TPA katika kuhakikisha meli hizi zinafanya kazi.”
Tukio hilo la makabidhiano limefanyika leo tarehe 06.09.2022 baada ya pande zote mbili kutia saini hati ya makabidhiano ya meli hizo tukio ambalo limeshuhudiwa na vyombo vya serikali ikiwemo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ofisi ya Mwanansheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kyela, na Diwani wa Kata ya Kajojomole katika bandari ya Kiwira.