Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akizungumza katika Jukwaa la Wakuu wa Nchi na Serikali la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRF2022) lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kigali nchini Rwanda.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika, Wakuu wa Taasisi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na Viongozi Wakuu Wastaafu mara baada ya kumalizika kwa Jukwaa la Wakuu wa Nchi na Serikali la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRF2022) lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kigali nchini Rwanda.
************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameshiriki Jukwaa la Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika katika Mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika wa Mwaka 2022 (AGRF 2022) unaofanyika Kigali nchini Rwanda.
Majadiliano katika Jukwaa hilo yameangazia namna nchi za Afrika zitakavyoweza kukabiliana na tishio la Usalama wa Chakula kutokana na sababu mbalimbali duniani kama vile mabadiliko ya tabia nchi, athari za Uviko 19 pamoja na migogoro baina ya mataifa duniani.
Akizungumza katika Jukwaa hilo ,Makamu wa Rais amesema mataifa ya afrika yanapaswa kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika bara hilo pamoja na kuungana mkono katika utumiaji wa rasilimali zilizopo ikiwemo nishati na gesi.
Makamu wa Rais amesema ajenda ya usalama wa chakula inapaswa kuendelea kujadiliwa katika mikutano mingine mbalimbali ikiwemo ile ya kikanda na Mkutano wa Umoja wa Afrika kwa sababu inagusa maisha ya wananchi ya kila siku.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameongeza kwamba migogoro iliopo katika mataifa mbalimbali barani Afrika inapaswa kukomeshwa ili kuruhusu wakulima waweze kuzalisha mazao kwa utulivu na amani.
Pia amesema mabadiliko katika kufikia teknolojia ya rafiki kwa mazingira yanapaswa kufikiwa kwa utaratibu maalum kwa kuzingatia hali za wananchi wa Afrika pamoja na kuyaasa mataifa makubwa ulimwenguni kuunga mkono na kushirikiana na nchi za Afrika katika kuleta mabadiliko hayo.
Akizungumzia jitihada za serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto zinazopelekea athari katika usalama wa chakula, Makamu wa Rais amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa katika kuinua sekta ya kilimo ikiwemo kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo ambapo tayari viwanda viwili kwaajili ya uzalishaji wa mbolea vinaendelea kujengwa, kuongezwa kwa bajeti ya sekta ya kilimo, kuanzisha skimu za umwagiliaji pamoja na ujenzi wa majengo ya kuhifadhia mazao.
Ameongeza kwamba serikali imeendelea kuboresha sera pamoja jitihada za kuwawezesha wakulima kupata mikopo katika taasisi za fedha kwa riba nafuu na kuondoa kodi zaidi ya 140 miongoni ya zilizokuwa zikiwaathiri wakulima.
Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya kilimo nchini Tanzania ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula barani Afrika.
Viongozi walioshiriki katika majadiliano hayo ni pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pamoja na Rais wa Niger Mohamed Bazoum. Viongozi hao wameeleza hatua mbalimbali ambazo mataifa yao yameendelea kuchukua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazohatarisha usalama wa chakula.