Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwasilisha Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile akizungumza wakati wa kikao cha uwasilishaji na upokeaji wa Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa kamati hiyo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022. Pembeni yake ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Dkt. Switbert Mkama.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakiwa katika kikao cha uwasilishaji na upokeaji wa Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa kamati hiyo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akifafanua jambo wakati wa kikao cha uwasilishaji na upokeaji wa Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa kamati hiyo na Ofisi ya Makamu wa Rais katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
Watalaamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwa katika kikao cha uwasilishaji na upokeaji wa Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa kamati hiyo na Ofisi ya Makamu wa Rais katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
**********************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema azma ya Serikali si ya kufungia viwanda badala yake imejikita katika kutoa elimu ili wawekezaji wafuate Sheria ya Mazingira.
Amesema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
Miongoni mwa masuala muhimu yaliyobainishwa yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ni pamoja na Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa hadhi ya Mamlaka.
Dkt. Jafo alisema ili nchi iendelee inahitaji wawekezaji hivyo kama kuna viwanda vinachafua mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais inavielekeza kurekebisha changamoto hizo ili uzalishaji uendelee.
“Ni kweli tunabaini baadhi ya viwanda kuchafua mazingira kwa njia ya hewa au majitaka lakini sisi kama Serikali hatukimbilii kuvifungia viwanda lakini tunachukua hatia ya kutoa elimu kwani kufungia viwanda kunasababisha watu wakose ajira na Serikali kukosa mapato kutokana na kodi,” alisema.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Waziri Jafo alisema alisema katika kutekeleza kazi ya kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 zipo kazi zilizofanyika ambazo ni kuifanyia uchambuzi Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 ili kubainisha masuala mapya yaliyojitokeza katika Sera mpya.
Alisema kuwa masuala muhimu yaliyobainishwa yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, uhawilishaji wa teknolojia na upatikananaji wa rasilimali fedha.
Pia alisema kuwa masuala mengine ni kuanzishwa kwa Kituo cha Kuratibu Hewa Ukaa Nchini na udhibiti wa biashara ya hewa ukaa ambayo mwongozo wake upo katika maandalizi.
Aidha, Waziri Jafo alisema uchafuzi wa mazingira umebainishwa kwa usimamizi wa kemikali katika hatua zote (life-cycle) na hifadhi ya mazingira katika shughuli za sekta ya gesi na mafuta.
Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 ilitungwa Mwaka 2004 kufuatia Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997. Sheria hii imekuwa ikifanyiwa marekebisho mbalimbali ili kuendana na wakati na kwa kuzingatia kwamba masuala ya mazingira ni mtambuka na ambayo yamekuwa yakibalidilika kulingana na wakati.
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ndio inayosimamia Sheria hiyo na ndani ya Sheria hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais amepewa mamlaka ya kutunga kanuni kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191.
Hivyo, kutokana na ukweli kwamba Sheria hiyo ni ya muda mrefu ipo haja ya kuihuisha ili iweze kuendana na wakati.