Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic, Mhe. Anne Beathe Tvinnereim amewasili nchini leo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 6 – 8 Septemba 2022 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula.
Akiwa nchini Mhe. Tvinnereim kwa nyakati tofauti, atakutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jaffo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde.
Aidha, Mhe. Tvinereim pia anataraji kutembelea miradi ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) pamoja na Mji wa Serikali (Mtumba) Jijini Dodoma ili kujionea maendeleo ya miradi sambamba na mikakati ya Serikali katika kufanikisha miradi hiyo.
Tanzania na Norway zinashirikiana katika sekta za elimu, afya, kilimo, uwekezaji, miundombinu, nishati, madini, tehama, utafiti, maboresho kwenye mifumo ya ukusanyaji wa kodi, uchangiaji wa bajeti kuu ya Serikali, misitu, demokrasia, haki za binadamu, usawa wa jinsia, utunzaji wa mazingira na ukuzaji wa sekta ya biashara.
Maeneo mengine mtambuka ya ushirikiano ni pamoja na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, utawala bora, usimamizi wa migogoro, amani na ulinzi.