Mkandarasi kutoka kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group Mhandisi Michael Masambwa akimuonesha Meneja wa vivuko TEMESA Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe kulia maeneo ya kivuko yanayoendelea kufanyiwa ukarabati wakati alipotembelea kukagua ukarabati wa kivuko hicho unaoendelea katika eneo la Pangani Mkoani Tanga. Kushoto ni Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir.
Muonekano wa kivuko cha MV. TANGA kinachoendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa katika fukwe ya Pangani Mkoani Tanga, kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa na tani 50 kinatarajiwa kukamilika ukarabati wake ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Mafundi kutoka kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group wakiendelea na kazi ya kukata mabati ambayo yatarudishiwa kwenye kivuko cha MV.TANGA na kuondoa yale ambayo tayari yamekwisha haribika hasa katika eneo yanapopaki magari na eneo la kukaa abiria. Ukarabati wa kivuko hicho unaendelea katika eneo la Pangani Mkoani Tanga na kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Meneja wa vivuko TEMESA Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe wa mwanzo akionyeshwa mabati yaliyokwishaondolewa na kukatwa katika kivuko cha MV.TANGA kinachoendelea ufanyiwa ukarabati mkubwa katika fukwe ya Pangani Mkoani Tanga. Nyuma yake ni Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir na anayemuonyesha ni Mkandarasi kutoka kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group Mhandisi Michael Masambwa. kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa na tani 50 kinatarajiwa kukamilika ukarabati wake ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
Meneja wa vivuko TEMESA Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe kulia, Mkandarasi kutoka kampuni ya Dar es Salaam Merchant Group Mhandisi Michael Masambwa katikati na Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir wakikagua baadhi ya vifaa (matirio) zinazotumika katika ukarabati wa kivuko cha MV. TANGA unaoendelea eneo la Pangani Mkoani Tanga, kivuko cha MV.TANGA kinatarajiwa kukamilika ukarabati wake ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO – TEMESA TANGA
……………………………
Na Alfred Mgweno – TEMESA TANGA
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini TEMESA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa vivuko nchini ambavyo muda wake wa kukarabatiwa umefika ili viendeelee kutoa huduma vikiwa katika hali ya usalama, katika muendelezo huo, kivuko cha MV TANGA kinachotoa huduma kati ya Pangani na Bweni Wilayani Pangani Mkoani Tanga ni miongoni mwa vivuko ambavyo vinaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho unaoendelea katika eneo la Pangani Mkoani Tanga, Meneja wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe amesema ukarabati huo unahusisha kuondoa mabati ambayo yamekwisha haribika sehemu za abiria na magari yanapopaki yakiingia ndani ya kivuko pamoja na chini ya kivuko, viti vya abiria, Kuweka vifaa vipya vya uokozi ikiwemo majaketi ya kujiokoa pamoja na maboya ya kujiokoa, kuondoa milango ya mbele na nyuma ya kivuko (ramps), kufunga viongoza kivuko vipya (navigation systems) pamoja na kupaka rangi kivuko hicho mara baada ya ukarabati wake.
‘’Mkandarasi yuko ndani ya muda wa utekelezaji wa mradi huu baada ya malipo ya awali na ameshaleta matirio zote za mabati yanayohitajika kwa ajili ya kubadilisha haya yaliyokwishakatwa, mabati haya yapo hapa eneo la mradi na tumetembea kuja kukagua na tunamuhamasisha mkandarasi ili aweze nae kukamilisha hii kazi ndani ya muda mfupi ili kivuko cha MV.TANGA sasa kiweze kurudi kusaidiana na chenzie cha MV. PANGANI II ambacho kwa sasa ndo kinatoa huduma katika eneo la Pangani Bweni’’. Alimaliza Mhandisi King’ombe.
Naye Mkuu wa Kivuko cha Pangani Mhandisi Abdulrahman Ameir akizungumza wakati wa ukaguzi huo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za vivuko nchini kwa kuendelea kuvifanyia ukarabati vivuko vyake kote nchini na kuahidi kusimamia kwa ukaribu kuhakikisha mkandarasi anamaliza kukarabati kivuko hicho kwa ufanisi na katika muda uliopangwa na kukirejesha kivuko hicho kutoa huduma haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa Mkandarasi anayefanya ukarabati huo, Dar es Salaam Merchant Group, kivuko cha MV.TANGA kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.