Na: Mwandishi Wetu
Wawakilishi wa Menejimenti ya Mamlaka inayosimamia Mawasiliano nchini Msumbiji akiwemo mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo Bw. Francisco Chate ambae aliongoza ujumbe huo walifika jijini Dar es salaam katika ziara ya kikazi ili kujifunza masuala ya Usimamizi wa Mawasiliano katika maeneo ambayo Tanzania imepiga hatua, hasa Usimamizi wa masafa, ubora wa huduma na Mawasiliano katika maeneo ya mipaka.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Bw. John Daffa akiongoza kikao-kazi na Ujumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano-Msumbiji INCM uliozuru TCRA kwa ziara ya Mafunzo Jumatatu Septemba 5, 2022. Picha na: TCRA
Ujumbe wa Menejimenti hiyo ulipokelewa Jumatatu tarehe 5 Septemba 2022 na Kaimu Mkurugenzi mkuu wa TCRA Bw. John Daffa ambae aliwapitisha wajumbe hao juu ya kazi za TCRA na kueleza dhamira ya TCRA kushirikiana nao kuwapa uzoefu muhimu utakaowezesha usimamizi thabiti wa huduma za Mawasiliano Msumbiji.
“Tuna uhakika ushirikiano huu ni muhimu katika kukuza sekta za Mawasiliano kwenye nchi zetu na bila shaka wataalam wetu watawapatia uzoefu mzuri wa namna sekta pana ya Mawasiliano inavyosimamiwa,” alisisitiza Daffa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili kiongozi wa ujumbe huo ambae ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Msumbiji mhandisi Francisco Chate alieleza kuwa wanayo matumaini makubwa juu ya uzoefu iliyonayo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania katika kusimamia teknolojia na huduma za Mawasiliano katika ukanda wa Afrika hasa kusini mwa jangwa la Sahara.
“Lengo letu ni kuhakikisha nchi yetu inaunganishwa vilivyo na Mawasiliano na ndio sababu ya ujio wetu Tanzania, tukiamini TCRA mnao uzoefu wa kutosha kutupatia maarifa zaidi ya namna tunavyoweza kusimamia na kuboresha huduma za Mawasiliano hasa simu na intaneti ” alisisitiza Mhandisi Chate.
Wengine katika ujumbe huo ni Bw. Edmundo Alberto Mkuu wa Idara ya Ufuatiliaji na Ubora wa Huduma na Bi. Feliciana Maquina Afisa katika Idara ya TEHAMA ambao wote walieleza kufurahishwa na namna Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilivyojidhatiti kusimamia sekta ya Mawasiliano kwa teknolojia ya kisasa.
Hii ni ziara ya pili kufanywa na Mamlaka hiyo kwa TCRA ikinuia kufanya mageuzi makubwa ya namna inavyosimamia huduma za Mawasiliano nchini humo ikiwemo kuboresha namna inavyosimamia ubora wa huduma na usambazaji wa huduma za Mawasiliano katika majimbo mbalimbali ya Msumbiji.