************************
Na Joseph Lyimo
“Baadhi ya jamii zinashindwa kukamilisha chanjo ya dozi ya UVIKO-19 kutokana na ubishi hivyo elimu wanapaswa kupatiwa kila mara japo wataalam wa afya wamewasihi mara nyingi kuwa inahitajika kumaliza dozi kamili ya UVIKO-19 ili uweze kupambana vyema na janga hilo,” anaeleza John Mathias mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara juu ya changamoto ya kumaliza dozi ya chanjo ya UVIKO-19.
Mathias anaeleza kwamba kwa mujibu wa wataalam wa afya mtu anapokuwa amepata chanjo ya dozi moja ya UVIKO-19 anakuwa hajakamilisha chanjo hiyo tofauti na yule ambaye amemaliza dozi ya pili ya chanjo hiyo kwa kurudia na kupata mara mbili.
Anasema kuwa wataalam wa afya wamekuwa wakieleza kwamba endapo mtu akipata chanjo ya Sinopharm au ya Pfizer anapaswa kumaliza dozi kamili kwa kurudia mara ya pili ila baadhi ya watu hawakamilishi dozi hiyo kwani wanachanjwa mara moja na kudhani kuwa wamekamilisha kinga yao.
“Elimu tunakuwa tunapata kuwa tunapaswa kukamilisha dozi kwa kumaliza chanjo hiyo kwa kurudia mara ya pili, ila sijui tatizo ni nini nadhani elimu iendelee kutolewa kwa baadhi ya watu ili waweze kukamilisha dozi zote mbili,” anasema Mathias.
Amewataka wataalam wa afya wasikate tamaa au kuvunjika moyo kwa baadhi ya watu wanaowapa elimu ya umuhimu wa kukamilisha chanjo ya pili na awakamilishi kwani jamii inapaswa kuelimishwa kila mara hadi wafahamu vyema.
Mkazi mwingine wa kata ya Shambarai wilayani Simanjiro, Elias Naidaha anasema kuwa yeye ni mfugaji aliyepata mara mbili chanjo ya UVIKO-19 baada ya kupatiwa elimu na wataalam wa afya.
“Mwaka 2021 nilipata chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm ambayo inapaswa kutolewa mara mbili ili kukamilisha dozi name ndivyo nilivyofanya kwani nilichanjwa mwezi Juni na kukamilisha dozi mwezi Julai mwaka jana,” anasema Naidaha.
Anasema changamoto iliyopo hadi kusababisha baadhi ya watu kutokuamilisha dozi ni kutokutambua kuwa ili uweze kukamilisha chanjo ya UVIKO-19 ni kumaliza dozi yote mbili endapo umepangiwa hivyo.
Anasema afya ni mtaji wa mtu hivyo jamii inapaswa kutambua kuwa ili kuhakikisha wanaishi maisha yao kama wanavyopaswa ni kuepuka mambo ambayo yanaepukika kwa kukamilisha dozi walizopangiwa na wataalam wa afya.
Hata hivyo, licha ya juhudi za serikali za kuhakikisha kila mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anapata chanjo ya kumkinga na virusi vya UVIKO-19 imebainika kuwa zaidi ya watu milioni 1.6 waliopaswa kupata dozi ya pili hawajakamilisha dozi hiyo.
Mtaalamu wa Wizara ya Afya kitengo cha elimu ya afya kwa umma uniti ya uhamasishaji, uelimishaji, ushirikishwaji wa jamii wakati wa dharura na matukio ya afya (RCCE) Juliana Mshama anasema kwamba watu hao hawakurudi kupata chanjo ya pili ili kukamilisha dozi yao.
Mshama anaeleza kuwa pamoja na mwamko wa wananchi kupata dozi ya kwanza ya chanjo ya UVIKO-19 mwamko ni mdogo kwa wale wanaorudi kukamilisha dozi na kuwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuhamasisha wananchi kurudi kwenye vituo vya afya kukamilisha dozi ya pili.
Mshama anasema Julai 31 mwaka 2020 watu 449,416 sawa na asilimia 26 ya watu milioni 1.7 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Pfizer hawakurudi, huku watu 325,982 sawa na asilimia 13 kati ya watu milioni 24 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm hawakurudi.
“Mwezi Agosti 14, 2022 watu 416,869 sawa na asilimia 24 kati ya watu milioni 1.7 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Pfizer na watu 455,952 sawa na asilimia 17 ya watu milioni 2.7 waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm hawakurudi,” anasema.
Mshama anasema kuwa watanzania waliopata chanjo kamili hadi sasa ni 15,960,643 sawa na asilimia 51.92 ya wananchi milioni 30.7 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea na kwamba wale ambao hawajakamilisha dozi hawahesabiki kama wamepata chanjo hadi watakapokamilisha chanjo hiyo.
“Hawa tunawaweka kwenye kundi la ambao hawajakamilisha dozi kama tujuavyo chanjo ni hiari ya mtu na kukamilisha dozi ya pili ni hiari yake uamuzi ni wake mwenyewe sisi tunachofanya ni kuwaelimisha na kuwahamasisha ili waone umuhimu wa kumaliza dozi,” anaeleza Mshama.
Anasema lengo la Serikali ni kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa watu zaidi ya 21 milioni sawa na asilimia 70 ya wananchi 30.7 milion wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ifikapo mwezi Desemba 2022.
Mtaalamu wa ufuatiliaji na mdhibiti wa magonjwa wa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo anaeleza kuwa endapo mtu atapata chanjo mara moja na hakumaliza dozi ya pili atakuwa hajapata chanjo kamili ya UVIKO-19.
Dkt Nzobo anasema kwamba inatakiwa mtu akipata chanjo ya UVIKO-19 anapaswa kushiriki chanjo ya pili ili kumaliza dozi kamili ya kupambana na janga hilo la UVIKO-19 kuliko kuchanja mara moja.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Dkt Aristidy Raphael anasema kwa upande wa eneo hilo hivi sasa hali hiyo haikuwepo kutokana na aina ya dozi waliyokuwa wanaitumia kutohitajika jamii kutumika mara mbili.
“Simanjiro tulitumia dozi aina moja ya Johnson Johson ambayo mtu akipatiwa chanjo kwa mara moja hapaswi kurudia tena hivyo kukamilisha dozi zao kwa wakati huu,” anasema Dkt Raphael.