Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Usalimishaji Silaha haramu kwa hiari . Uzinduzi huo umefanyika Septemba 5, 2022 jijini Dodoma katika Viwanja vya Mashujaa. (Picha na Hassan Mndeme)
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Usalimishaji Silaha haramu kwa hiari . Uzinduzi huo umefanyika Septemba 5, 2022 jijini Dodoma katika Viwanja vya Mashujaa. (Picha na Hassan Mndeme)
Mwakilishi wa Kituo cha Kuzuia na kudhibiti silaha ndogondogo na nyepesi kwa nchi za maziwa makuu na pembe ya Afrika (RECSA) Dkt Philip Ouma akizungumza katika uzinduzi wa Kampeni ya Usalimishaji Silaha haramu kwa hiari . Uzinduzi huo umefanyika Septemba 5, 2022 jijini Dodoma katika Viwanja vya Mashujaa. (Picha na Hassan Mndeme)
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini akizungumza na na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura baada ya uzinduzi wa Kampeni ya Usalimishaji Silaha haramu kwa hiari . Uzinduzi huo umefanyika Septemba 5, 2022 jijini Dodoma katika Viwanja vya Mashujaa. (Picha na Hassan Mndeme)
*****************
Na. A/INSP Frank Lukwaro
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Jumanne Sagini amewataka Wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sharia kutumia vyema msamaha uliotolewa na Serikali wa kipindi cha miezi miwili kusalimisha silaha haramu kwa hiari katika vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, ofisi za watendaji wa Serikali za mitaa na vijiji.
Sagini aliyasema hayo Septemba 5, 2022 jijini Dodoma wakati akizindua Kampeni maalumu ya Usalimishaji wa silaha ambayo ina lengo la kuhamasisha wananachi kusalimisha silaha wanazomiliki isivyo halali kwa hiari katika kipindi cha miezi miwili ikiwa na kauli mbiu isemayo “Silaha haramu sasa basi,Salimisha kwa hiari”.
Sagini alisema uzagaaji wa silaha haramu umekuwa chanzo cha vifo vya watu katika maeneo mbalimbali kutokana na wamiliki wake kuzitumia vibaya ikiwemo kwa kutokujua misingi na matumizi yake.
Aidha aliongeza kuwa katika kipindi hicho msamaha hakuna msalimishaji atakayechukuliwa hatua zozote wala kukamatwa kwa kuwa jambo hilo lipo kisheria na Serikali imeridhia ili kukusanya silaha ambazo zipo katika jamii kinyume cha sharia.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura alisema Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa yenye lengo la kuzuia uzagaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi ambapo kila mwaka Serikali imekuwa na utaratibu wa kutangaza msamaha kwa watu wanaomiliki silaha kinyume na sharia.
IGP Wambura alisema baada ya silaha hizo kukusanywa zitateketezwa bila kificho mwezi Novemba mwaka huu ili jamii ione na kutambua jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine katika udhibiti wa silaha ndogondogo na nyepesi.
Naye Mwakilishi wa Kituo cha kikanda cha kuzuia na kudhibiti silaha ndogondogo na nyepesi kwa nchi za maziwa makuu na pembe ya Africa (RECSA) Dkt. Philip Ouma aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kutekeleza maazimio ya RECSA katika udhibiti wa silaha ndogondogo na nyepesi ambapo mafanikio yake ni pamoja na nchi za ukanda wa maziwa makuu na pembe ya Afrika kuendelea kuwa salama.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Viongzoi mbalimbali wa Serikali, Asasi za kirai, Viongozi wa dini, Polisi Kata,Watendaji wa mitaa, Wenyeviti wa Serikali za mitaa na Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.