Katibu tawala msaidizi kitengo cha rasilimali watu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa biashara na maafisa afya Jijini Mwanza
Mkurugenzi wa udhibiti ubora kutoka TBS Lazaro Msasalaga akizungumza na waandishi wa habari
Maafisa afya, biashara viongozi wa TBS na mgeni rasm wakiwa kwenye picha ya pamoja
Maafisa afya na biashara wakiwa kwenye mafunzo ya siku moja ya kujengewa uwezo juu ya sheria, kanuni na miongozo inayohusika katika utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano baina ya TBS na Tamisemi
**********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa biashara na maafisa afya wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri za Wilaya na Manispaa kuhusu sheria,kanuni na miongozo inayohusika katika utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano baina ya TBS na Mamlaka za Serikali za mitaa (TAMISEMI).
Mafunzo hayo ya siku moja yametolewa leo Septemba 5, 2022 katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la TMDA Jijini hapa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dk. Athumani Yusuphu Ngenya, Mkurungenzi wa udhibiti ubora kutoka katika Shirika hilo Lazaro Msasalaga, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yaliyoainishwa katika kanuni ya mashirikiano.
Amesema TBS inatambua umuhimu wa watumishi wa umma katika Halmashauri za Mikoa yote ya Tanzania hususani maafisa afya na biashara kuwa na mchango mkubwa katika kulinda ubora,usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi ili kulinda afya ya walaji pamoja na kuleta tija kwenye uchumi.
Msasalaga amesema TBS imekuwa ikifanya shughuli za ukaguzi na udhibiti kwa kushirikiana na watumishi kutoka katika Ofisi za Halmashauri huku akisema wanamchakato endelevu wa kuendesha mafunzo kwa watumishi wa tamisemi.
Kwa upande wake Afisa Afya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sophia kiluvya, amesema mafunzo hayo yatamuwezesha kujua mbinu za kutambua bidhaa za vyakula ambazo siyo salama.
Naye Afisa biashara kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Antony Esaya, amesema mafunzo hayo yamemuongezea wigo wa kutoa elimu kwa Wananchi juu ya kuleta bidhaa ambazo ni salama.
Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu tawala Mkoa wa Mwanza Elikana Balandya,Katibu tawala msaidizi kitengo cha rasilimali watu Daniel Machunda, amewaasa maafisa hao kutotumia kanuni na sheria wanazopewa kama fimbo ya kuwachapia Wananchi badala yake wazitumie kwaajili ya kuwaelimisha ili walete bidhaa bora sokoni na mlaji apate bidhaa ambazo hazitakuwa na madhara kwenye afya yake.