Na Mwandishi Wetu
Ili kupata manufaa ya huduma za teknolojia ya Habari na Mawasiliano wakazi wa Morogoro wamesisitizwa kutumia fursa za mtandaoni kujinufaisha katika kukuza shughuli za kilimo, ujasiriamali, elimu na ukuzaji tija katika Maendeleo binafsi na ya taifa.Afisa wa TCRA Bi. Rehema Kihiyo akiwahudumia wajasiriamali wadogo katika soko la gulio la SabaSaba, mjini Morogoro. PICHA: TCRA
Hayo yalibainishwa na Afisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Robin Ulikaye wakati akitoa elimu kwa wananchi waliofika kujipatia mahitaji mbalimbali katika soko la mnada wa Jumapili ‘gulio’ ambalo hufanyika kila Jumapili mjini Morogoro eneo la Sabasaba.
Amesema Mamlaka ya Mawasiliano ilifika kwenye soko hilo la mnada kuwapa wananchi elimu juu ya matumizi ya huduma za Mawasiliano ikiwemo fursa zinazopatikana katika anga la kimtandao “the cyber space”. Ulikaye aliwaeleza wananchi kuwa TCRA kupitia kampeni yao ya Kwea Kidijitali wanalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu stahiki ya matumizi sahihi na salama ya mtandao, ikiwa ni Pamoja na kung’amua fursa zilizomo kwenye anga la kimtandao.
“Mitandao ina fursa lukuki zikiwemo kupata elimu kwa wanafunzi, kujifunza na kupata masoko ya shughuli zako za ujasiriamali, kilimo, biashara na nyingine nyingi zinazokuwezesha Kukwea Kidijitali; TCRA tunasisitiza unapotumia mitandao hiyo hakikisha umehakiki usajili wa laini zako za simu kwa kubofya *106#, kisha ufuate maelekezo,” alisisitiza Ulikaye.
Ulikaye alibainisha kuwa unapobaini namba usiyoifahamu fika kwa mtoa huduma wako na kuiondoa mara moja. Aidha, alisisitiza kuwa kutoa taarifa kwa kikosi kazi kinachohusisha Jeshi la Polisi, mtumiaji wa huduma za Mawasiliano mara anapopokea ujumbe wa kitapeli, anapaswa kuiripoti namba iliyomtumia ujumbe huo kwenda namba 15040, huduma aliyosisitiza kuwa haitozwi gharama zozote kwa mtumiaji wa huduma anaetoa taarifa.
Amesema katika kazi hiyo ya kuwaelimisha wananchi kuhusu Mawasiliano TCRA iliambatana na watoa huduma wote wa Mawasiliano ya simu Pamoja na Jeshi la Polisi, kwa shabaha ya kuwapatia wananchi wa Morogoro huduma zilizokamilika kuhusu Mawasiliano.
Akizungumzia ushiriki wa Jeshi la Polisi kwenye kampeni hiyo ya elimu kwa umma, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ambae pia anasimamia Kitengo cha Mitandao Fadhili Ally Magombela alibainisha lengo la Jeshi hilo kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwa kina kuhusu usalama wao wanapokuwa kwenye anga la mtandao.
“Maisha kwenye mtandao hayatofautiani sana na Maisha katika ulimwengu wa kawaida, kwa hiyo tunapenda kuwasisitiza wananchi, wakati wote kuhakikisha wanakuwa makini wanapokuwa kwenye mazingira ya kimtandao, kwa kuwa uhalifu huko ni halisi, aidha tunawaasa wananchi ukitapeliwa au kunusurika katika utapeli mtandaoni hakikisha unatoa taarifa katika kituo cha Polisi Jirani yako ili hatua zichukuliwe” alibainisha Afisa huyo wa Polisi.