Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya ya Singida, Bahati Colex (kulia) akizungumza katika semina ya wenyeviti wa mabaraza ya Kata wa Manispaa ya Singida iliyohusu mabadiliko ya sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi iliyofanyika jana Septemba 3, 2022 ukumbi mdogo wa baraza hilo mjini hapa. Kushoto ni Mwanasheria wa Manispaa ya Singida, Burton Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi na mmoja wa wawezeshaji wa semina hiyo.
Mwanasheria wa Manispaa ya Singida, Burton Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi akioa mada kwenye semina hiyo.
Mshiriki wa Semina hiyo, Saidi Siri Saidi akisisitiza jambo.
Semina ikiendelea. Kutoka kushoto ni Mzee Ramadhani Mdanku kutoka Kata ya Mandewa, Mzee Hassan Mlowosha kutoka Kata ya Misuna, Mzee Jumanne Wahija kutoka Kata ya Kisaki na Mzee Saidi Lissu kutoka Kata ya Mtamaa.
Mwanafunzi wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Deodatus Marcel akichangia jambo kwenye semina hiyo.
Taswira ya semina hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi la Kata Manispaa ya Singida, Abdallah Mohamed Muhandi akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Afisa Mtendaji Kata ya Mungumaji, Bakari Ntandu akichangia jambo kwenye semina hiyo.
Afisa Mtendaji Kata ya Majengo, Edward Salimu akizungumza kwenye semina hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza la Usuluhishi Kata ya Utemini, Benard Maira akichangia jambo kwenye semina hiyo.
********************
Na Dotto Mwaibale, Singida.
SERIKALI imefanya marekebisho ya Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa migogoro ya ardhi namba 216, ambapo mabaraza ya kata yameondolewa uwezo wa kusikiliza mashauri ya ardhi kama yalivyo kuwa yakifanya awali.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya ya Singida, Bahati Colex, alisema hayo leo wakati wa semina ya wenyeviti wa mabaraza ya kata wa Manispaa ya Singida kuhusu mabadiliko ya sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Alisema marekebisho hayo ya sheria yanalenga kuboresha utoaji haki hasa ukizingatia kuwa jukumu hili yalipewa mabaraza ya kata ambayo kimsingi wajumbe wake si wataalamu wa sheria, hali iliyosababishwa kufutwa kwa maamuzi yao mengi kutokana na makosa ya kisheria kama kutotimia kwa akidi.
Colex alisema kufuatia marekebisho hayo ya sheria ambayo yalianza kutumika rasmi 11 Oct,2021mabaraza hayo ya kata yamepewa jukumu la usuluhishi tu ambao utatakiwa kufikiwa ndani ya siku 30 kutoka siku shauri lilipofunguliwa.
Alisema usuluhishi ukishindikana mabaraza ya kata yatatoa cheti cha usuluhishi ili wadaawa waweze kufungua shauri lao kwenye baraza la ardhi na nyumba wilaya na kwamba hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 13(2),13(4) vya Sheria ya mahakama za utatuzi wa migogoro ya ardhi kama ilivyorekebishwa na Kifungu cha 45 cha Sheria no.5/2021 “The Written Laws (miscellaneous Amendments) (No.3) Act, 2021.
“Kifungu cha 45 cha sheria hii kimerekebisha kifungu cha 13 (2) na kuyapa mabaraza ya kata jukumu la usuluhishi tu badala ya kusikiliza kesi na kutoa hukumu, sasa mabaraza ya kata yanapaswa kusuluhisha mgogoro wa ardhi kati ya wadaawa ndani ya siku 30 kwa mujibu wa Kifungu cha 13 (4),”alisema.
Colex alisema kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya sheria mashauri yote ya ardhi yataanzia kwenye mabaraza ya kata bila kujali thamani ya ardhi husika, Kifungu cha 13 (4) kinaeleza kuwa mabaraza ya ardhi na nyumba wilaya halitasikiliza shauri lolote la ardhi mpaka baraza la kata lithibitishe kuwa limeshindwa kusuluhisha.
Alisema Baraza la Kata likishindwa kuwasuluhisha wadaawa litatoa cheti au hati ya usuluhishi ambapo wadaawa watakuwa na nafasi ya kufungua shauri lao la ardhi katika baraza la ardhi na nyumba wilaya.
Aidha, ikiwa siku 30 zitapita toka lalamiko lilipopelekwa baraza la kata bila kusuluhishwa, mlalamikaji anaruhusiwa kufungua shauri lake mbele ya baraza la ardhi na nyumba wilaya bila hata kuwa na cheti cha usuluhishi.
Aliongeza kuwa sheria hiyo pia inampa mamlaka Waziri wa Sheria akishirikiana na Waziri wa Ardhi kutengeneza kanuni zitakazo simamia uendeshaji wa usuluhishi mbele ya mabaraza ya kata, Kifungu cha 13 (5) kama kilivyofanyiwa marekebisho na Kifungu cha 45.
“Sheria hii kupitia Kifungu cha 46 na 47 imefuta Kifungu cha 15 ambacho ni sawa na Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mabaraza ya kata ambavyo vinahusu uwezo wa mabaraza ya kata kusikiliza mashauri ya ardhi yasiyo zidi thamani ya milioni tatu, Imefuta Kifungu cha 16 ambacho kinahusu mamlaka ya mabaraza ya kata yanaposikiliza mashauri ya ardhi, Imefuta Kifungu cha 20 kinachohusu rufaa na muda wa kukata rufaa, na imefuta Kifungu cha 21 kilichokuwa kinampa nguvu waziri kutengeneza kanuni za kuendesha rufaa kutoka baraza la kata kwenda baraza la ardhi na nyumba wilaya,” alisema.
Colex alisema kuhusu mashauri ya ardhi yaliyofunguliwa kabla ya 11 Oct,2021 mbele ya Mabaraza yakata a kabla ya mabadiliko haya ya sheria yataendelea kwa utaratibu wa zamani na yatatolewa hukumu.
“Kwakuwa mabadiliko haya ya sheria yalianza 11 Oct, 2021, mashauri yote yaliyofunguliwa baada ya mabadiliko haya ambayo yanasikilizwa badala ya kusuluhishwa yanasikilizwa kimakosa mbele ya mabaraza hayo ya kata kwakua hayana mamlaka ya kusikiliza na kutoa hukumu hivyo mashauri hayo yanapaswa kusuluhishwa tu, na kwa yaliyotolewa hukumu basi hukumu hizo zitakuwa batili kwenye macho ya sheria kwakua zinatokana na mabaraza yasiyo na mamlaka kisheria,” alisema.
Mwanasheria wa Manispaa ya Singida, Burton Mahenge, alisema wajumbe wa Baraza la Kata wanapomaliza muda wao wa miaka mitatu wawe wanatoa taarifa mapema ili kutoa fursa kufanyika mchakato wa kupata wajumbe wapya.
Mahenge alisema wajumbe wanapochelewa kutoa tangazo la kumaliza muda wao kunasababisha uchelewaji wa usikilizwaji wa mashauri.
Nao wenyeviti wa kata Manispaa ya Singida walilishukru Baraza la Ardhi Wilaya ya Singida kwa kuitisha semina hiyo ambapo walisema mambo waliyofundishwa yatawajengea uelewa zaidi hasa baada ya serikali kufanya mabadiliko ya Sheria za mahakama za utatuzi wa migogoro ya Ardhi.
Walisema mafunzo hayo yatawawesesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuacha kufanya kwa mazoea hali itakayowezesha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Aidha, waliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaongezea posho ya kukaa kwenye vikao vya Baraza la Kata ambapo walisema kiwango cha Sh.1000 kinachotolewa kwa kikao kimoja hakitoshelezi kabisa kwakuwa baadhi yao wamekuwa wakitoka maeneo ya mbali. na kuwa kimepitwa na wakati.