Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akimsikiliza Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concar wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Viongozi hao walikutana ili kuzungumza juu ya ushirikiano wa kisekta baina ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Daoglas Foo baada ya mazungumzo yao kuhusu ushirikiano wa kisekta baina ya nchi hizo mbili. Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
……………………………………
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa nchi za Uingereza na Singapore kwa nyakati tofauti kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya nishati.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Septemba 2, 2022 katika ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam huku yakihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Wizara na walioongozana na mabalozi hao.
Kwenye mazungumzo yake na Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. David Concar, viongozi hao wamejadili maeneo ya ushirikiano ambayo ni pamoja na kujengea uwezo wataalamu hususani katika kusasisha mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya umeme nchini (Power System Master Plan), kubadilishana uzoefu katika eneo la umeme na katika utekelezaji wa miradi ya umeme wa nishati jadidifu.
Waziri Makamba amewakaribisha wawekezaji wa nchini Uingereza kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme (Independent Transmission Providers) pamoja na miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu.
Naye Balozi Concar amesema Serikali ya Uingereza ipo tayari kutoa msaada kwa Tanzania kwenye masuala ya kiufundi. Vivyo hivyo amesema Serikali hiyo ina nia ya kushirikiana na Tanzania kwenye masuala ya nishati bora ya umeme wa kupikia (electronic cooking).
Kwa upande mwingine, wakati wa mazungumzo baina ya Waziri Makamba na Balozi wa Singapore Daoglas Foo viongozi hao wamejadili kuhusu uwezekano wa Tanzania kununua mafuta kutoka Singapore na ushirikiano katika miradi ya nishati jadidifu.
Balozi Foo amemtaarifu pia Waziri Makamba kuwa Serikali ya Singapore tayari imeshaanza kufanya mazungumzo na wafanyabishara wa Tanzania kwaajili ya kuwa na makubalino ya biashara, na kuongeza kuwa mwaka 2023, Singapore itatuma watalaamu wake kuwa Tanzania ili kujadili maeneo mbalimbali ya uwekezaji na ushirikiano.