Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.Amos Makalla wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Swallow investment Ltd kilichopo Tegeta Jijini Dar es Salaam. Afisa Mazingira NEMC Bw.Erick Fussi akimuonesha Waziri Jafo baadhi ya Mifuko ambayo wameikamata katika kiwanda cha Swallow investment Ltd mara alipofanya ziara katika kiwanda hicho kilichopo Tegeta Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo akimisikiliza Afisa Rasilimali Watu wa kiwanda cha Swallow investment Ltd kilichopo Tegeta mara baada ya kutembelea kiwanda hicho leo Septemba 2,2022, ambacho kinazalisha Mifuko iliyokatazwa ambapo zaidi ya Tani 41 za Mifuko hiyo zimekamatwa.Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake kwenye Kiwanda Swallow investment Ltd kilichopo Tegeta leo Septemba 2,2022 Jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya Waziri Jafo kwenye Kiwanda Swallow investment Ltd kilichopo Tegeta Jijini Dar es Salaam.Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla wakati walipotembelea kiwanda cha Swallow investment Ltd ambacho kinazalisha mifuko ambayo imepigwa marufuku.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo ametoa muda wa siku 7 kwa Wafanyabiashara na Wananchi Wenye Mifuko ya plastiki iliyokatazwa kuisalimisha kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kupitia kikosi kazi au Kwenye Kiwanda walichochukulia Mzigo.
Pia Waziri Jafo amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Amos Makalla kwa Operesheni ya kukamata Mifuko hiyo.
Waziri Jafo ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara kwenye Kiwanda Swallow investment Ltd kilichopigwa faini ya Shilingi Milioni 100 kwa kosa la kuzalisha Mifuko iliyokatazwa ambapo zaidi ya Tani 41 za Mifuko hiyo zimekamatwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Jafo amempongeza RC Makalla kwa kufanikisha kukamatwa kwa Shehena ya Mifuko hiyo kupitia Operesheni aliyotangaza na kuelekeza Mikoa mingine kuiga mfano wa Mkoa wa Dar es salaam.
Aidha Waziri Jafo amemtaka Mmiliki wa Kiwanda hicho kulipa faini aliyopigwa ndani ya siku 14 na kuhakikisha anatoa gharama zote za uteketezaji wa mzigo uliokamatwa na Mifuko iliyoingizwa sokoni ahakikishe anaikusanya.
Pamoja na hayo Waziri Jafo ameelekeza Kiwanda hicho kuanza mchakato wa kupata cheti Cha tathimini ya athari za mazingira na kuzitaka Mamlaka za TRA, TBS, NSSF na Taasisi nyingine kufika kiwandani hapo kuona Kama wanazingatia taratibu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) alipozungumza amewataka wawekezaji kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, pamoja na Kanuni zake ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea ikiwemo kutozwa faini au kuchukuliwa hatua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amemshukuru Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Mazingira kwa kumuunga mkono kwenye Operesheni hiyo.