Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi katika eneo la Mitamba Kibaha mkoani Pwani Septemba 1,2022, eneo ambalo limevamiwa na wananchi hao. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Anjeline Mabula akizungumza na wananchi katika eneo la Mitamba Kibaha mkoani Pwani Septemba 1,2022, eneo ambalo limevamiwa na wananchi hao. Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki akizungumza jambo na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Anjeline Mabula wakati walipofanya ziara ya kutembelea shamba la Mitamba Kibaha mkoani Pwani Septemba 1,2022 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge akizungumza na wananchi wa eneo la Mitamba mara baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki pamoja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Anjeline Mabula kufanya ziara ya kutembelea shamba la Mitamba ambalo limevamiwa na baadhi ya wananchi na kujenga makazi yao.Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Sarah Msafiri akizungumza na wananchi wa eneo la Mitamba mara baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki pamoja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Anjeline Mabula kufanya ziara ya kutembelea shamba la Mitamba ambalo limevamiwa na baadhi ya wananchi na kujenga makazi yao. Wananchi wa eneo la Mitamba Kibaha mkoani Pwani wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki baada ya kutembelea shamba la Mitamba ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) lililovamia na baadhi ya wananchi. Waziri Ndaki aliongozana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Anjeline Mabula pamoja na uongozi wa mkoa wa Pwani ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Abubakari Kunenge.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
******************
NA MWANDISHI WETU, PWANI
Serikali imechoshwa na mauziano ya ardhi yasiyofuata utaratibu kwa wananchi, na imepanga kuwachukulia hatua wale wote wanaosababisha migogoro hiyo kwa kuanza na watumishi wasio waaminifu pamoja na wavamizi Ili kila mmoja apate anachostahili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Anjeline Mabula (Mb) alipotembelea shamba la Mitamba Kibaha ambalo lipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusimamiwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) siku ya tarehe 01/09/2022.
Mhe. Mabula amesema katika kutatua mgogoro wa eneo lililovamiwa la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kuweza kutenda haki, Serikali iliamua kuunda Kamati ambapo iliwahoji wananchi 1,156 katika mitaa ya Lumumba na mkombozi na ilibaini kuwa watu wengi wamekuwa wakiuziana viwanja kinyume na sheria kwani Migogoro mingi inasababishwa na ununuzi unaofanywa kwa haraka na amewataka wananchi kuacha njia za mkato na wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Natoa onyo kwa viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa kuacha mara moja kujivika madaraka na kuvunja sheria bila sababu kwa kugawa ardhi ambayo ni kinyume na sheria na hawana mamlaka nayo katika nafasi ambazo wamepewa, kufanya hivyo ni kufanya kosa na sheria itafuata mkondo wake, na watu waliotajwa na wananchi mbele ya kamati kuwa wanahusika na magenge ya utapeli na vinara wa kuwauzia wageni ardhi ndani ya eneo la Wizara ya Mifugo na uvuvi, orodha yao ipo nao wachukuliwe hatua kama makundi mengine ya waharifu.
“Namuelekeza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani kufuata taratibu za kisheria kufuta hati za mashamba manne zilizotolewa kwenye shamba la Mitamba, vilevile namuelekeza Mkurugenzi wa upimaji na Ramani kufuta Ramani zote ambazo hazijafuata utaratibu, vibali vyote vya ujenzi na vilevile watumishi wote waliotufikisha hapa washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.” Alisema Mhe. Mabula
Aidha katika ziara hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alisema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipewa shamba la hekta 4,000 na Wizara ilikubali kuipatia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kiasi cha hekta 2,963 bila malipo yeyote na Wizara ikabaki na hetka 1,037. Pamoja na kugawa eneo hilo bado kuna watu wamevamia kile kipande kidogo kilichobaki.
“Siku ya leo tunafurahi kwamba jambo la mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na taasisi yetu ya chanjo linaelekea mwishoni, nichukue nafasi hii kukupongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Mkuu wa Mkoa kwa kuunda timu ambayo ndani yake wapo wataalamu ambao wamebobea kwenye mambo ya ardhi na wanauzoefu wa kutosha kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya ardhi. Namuomba mkuu wa Mkoa kuwachukulia hatua wale wote waliovamia eneo la Wizara. Eneo lililotolewa kwenye Halmashauri ligawanywe kwa utaratibu wa Halmashauri na eneo lililobaki tutalilinda.”
“Nimuelekeze Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) washirikiane na Halmashauri kuweka mipaka eneo lote la hekta 1,037 lililobaki ili watakaoingia wajulikane kabisa na kuchukuliwa hatua. Kwa kufuata sheria tunaweza kuishi kwa amani na utulivu.” Alisema Mhe. Ndaki
Katibu wa kamati iliyoundwa kwa ajili ya kutatua mgogoro huo ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Ndg. Hussein Iddi alisema kuwa walitumia vigezo mbalimbali kuweza kubaini watu waliovamia eneo hilo ambavyo ni pamoja na; kupata historia ya eneo husika, kubaini hali halisi ya uwekezaji ndani ya eneo hilo, kubaini wananchi waliomo ndani ya eneo na jinsi walivyoingia kwenye eneo hilo, kubaini vinara wa utapeli na uuzaji wa ardhi, kubaini sababu za uvamizi pamoja na kushauri na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kutatua mgogoro huo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge ameahidi kutenda haki na kuto muonea yeyote kwenye kuwachukulia hatua wale wote waliovamia eneo hilo na yote yaliyoagizwa kwenye mkutano ni salamu kwa wanaosababisha migogoro ya Ardhi kwa Mkoa wa Pwani na kwa upande wa watumishi wa Serikali waliosababisha mgogoro huo, mamlaka zao za nidhamu ziwachukulie hatua kwa mujibu wa sheria.
Mwaka 1982 Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliwasilisha ombi kwenye ofisi ya Mkoa wa Pwani wapatiwe eneo la kuanzisha shamba la Mitamba kwa ajili ya kuhudumia wafugaji wa kanda ya mashariki. Mkoa wa Pwani ulitoa hekta 4,000 ndani ya hekta hizo kuna wananchi 1,557 walikuwa wanaishi katika vijiji vya Pangani, Vikawe na Mpiji waliombwa kuondoka na walilipwa fidia kwa awamu tofauti tofauti kuanzia mwaka 1988 hadi 1992.