Na Mwandishi wetu, Babati
MAGARI 22 yanayobeba wanafunzi wa shule kwenye Wilaya za Babati na Kiteto Mkoani Manyara yamekaguliwa ubora wake wakati huu wa maandalizi ya kufunguliwa shule.
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Manyara, (RTO) Mrakibu wa Polisi (SP) Georgina Richard Matagi ameongoza ukaguzi huo wa magari hayo 22 ya shule yanayobeba wanafunzi.
Matagi amesema katika magari hayo 22 yaliyokaguliwa, kwenye Wilaya ya Babati yamekaguliwa magari 20 na wilaya ya Kiteto yamekaguliwa magari mawili.
“Kati ya magari hayo, 14 yametolewa namba za usajili baada ya kutwa na ubovu ili kwenda kurekebishwa na yakikamilisha ndiyo yatarudishiwa namba zao,” amesema RTO Matagi.
Amesema magari sita yamekutwa na ubora wa kubeba wanafunzi na kuruhusiwa kwenda kuendelea na shughuli za kubeba wanafunzi wa shule zao.
Amesema katika ukaguzi huo, wamebaini kwamba magari mawili ya kubeba wanafunzi hao hayakuwa na leseni ha usafirishaji.
“Ukaguzi huo umeambatana na utoaji elimu kwa wamiliki na madereva wa vyombo hivyo lengo ni kuwakumbusha wajibu wao madereva na wamiliki,” amsema RTO Matagi.
Amesema lengo ni kuhakikisha magari yanayobeba wanafunzi yanakaguliwa na kubaini ubora wao ulivyo kabla shule hazijafunguliwa jumatatu ijayo ya September 5
Katika ukaguzi huo RTO Matagi akiwa mjini Babati ameshirikiana na Msaidizi wake ASP Mahenda Kera na DTO Babati ASP James Makumu na Afisa mfawidhi wa LATRA Joseph Michael.