*******************
• AWATAKA WASANII KUZINGATIA MASLAHI YAO
Wasanii wametakiwa kuingia mikataba yenye tija na wasambazaji wa kazi za sanaa ili waweze kunufaika na kazi zao.
Hayo yamesemwa leo Septemba 01, 2022 na mtayarishaji na muandaaji mkongwe wa muziki nchini P-Funk “Majani” wakati akiongea na washiriki wa mafunzo ya muda mfupi yanayoendelea katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa udhamini Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na BASATA, TaSUBa pamoja na Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi (KISUVITA).
“Wasanii tuwe makini na mikataba tunayosaini na makampuni hasa mikataba inayomfunga msanii kwa muda mrefu,” alisema Majani.
Aidha P-Funk amewaeleza wasanii hao kuwa sio lazima wote wawe wanamuziki wengine wanaweza kujikita katika utayarishaji na uzalishaji wa muziki au kuwa mameneja wa wasanii ili kuhakikisha sanaa nchini inazidi kukua na kuimarika.
Mkongwe huyo katika utayarishaji na uzalishaji wa muziki nchini amewataka wasanii wajitaidi kupambana kivyao katika kuuza au kusambaza kazi za sanaa kuliko kuingia mikataba inayowanyonya ambayo kwa msanii inakua haina maslahi.
Aidha amewataka wasanii mbali na sanaa wawekeze katika shughuli nyingine za kiuchumi ili kujiongezea kipato na wasitetereke kimaisha.
P-Funky amesema kupitia uzoefu wake wa muda mrefu katika muziki yuko tayari kuwasaidia wasanii hasa wanaochipukia ili kuboresha na kukuza sanaa zao ili waweze kuwa watunzi na waimbaji wazuri wa muziki.
Mafunzo hayo yanahusisha wasanii 38, ambao 27 ni wasanii walioshiriki Shindano la “Taifa Cup Music Challenge” 2021, watano ni washindi wa Shindano la Bongo Star Search 2021 na walimbwende sita ambao wanajiandaa kushiriki Mashindano ya Dunia ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi 2022 (Miss & Mr Deaf International – MMDI).