Na John Walter-Manyara
Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani wa Jeshi la polisi Mkoa wa Manyara Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SP Georgina Richard Matagi amewaagiza wamiliki na watumiaji wa magari yanayotumika kubeba wanafunzi kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Ameyasema hayo Agosti 30,2022 wakati wa ukaguzi wa magari ya shule katika Wilaya ya Babati ambapo amesisitiza madereva kufuata sheria za barabarani ikiwa ni pamoja na kudhibiti mwendo kasi ili kulinda usalama wa wanafunzi.
Afisa huyo wa jeshi la polisi amesisitiza watumiaji wa magari ya shule kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani na kuepuka kutumia magari mabovu ili kuepusha ajari zinazoweza kuzuilika.
Mkuu huyo wa kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Manyara amesema wamebaini Magari katika baadhi ya shule ni mabovu huku mengine yakibainika kuwa na mfumo mbovu katika breki jambo ambalo ni hatari na kwamba yanatakiwa kurudishwa kwa ajili ya ukaguzi tena kabla ya shule kufunguliwa.
Hata hivyo magari yote yaliyokutwa na kasoro yamefunguliwa namba hadi yatakapokuwa sawa.
Ukaguzi huo ambao unafanyika kwa siku tano unahusisha wilaya zote tano za mkoa wa Manyara Mbulu,Babati,Kiteto,Hanang na Simanjiro.
Amewataka wamiliki wa shule hizo kuhakikisha madereva wanakuwa na umri wa kuanzia miaka 35-60 na magari kuwa na rangi ya njano kwa mujibu wa utararibu.
Aidha amewataka madereva wa magari ya wanafunzi Mkoani hapa kuepuka mwendo kasi ili kuepuka ajali.
Kwa upande wake Meneja mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Manyara Joseph Michael amesema zoezi la ukaguzi wa magari litakuwa endelevu ambapo amewataka madereva wanaoendesha magari mabovu kutoa taarifa sehemu husika ili wamiliki waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Michael amesema lengo la ukaguzi huo ni kuimarisha usalama hasa kwa wanafunzi barabarani kuepusha ajari zinazochangiwa na ubovu wa magari pamoja na uzembe wa madereva.
Nao Madereva wa magari yanayobeba wanafunzi wameahidi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa ili kuimarisha usalama wa wanafunzi.