Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi akizungmza na Wahifadhi wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka ambapo amewataka mafunzo watakayoyapata wayatafsiri kwa vitendo.
Baadhi ya Wenyeviti wa Kanda za Kiikolojia wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahifadhi katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka.
Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Sekretarieti ya Mafunzo akizungmza ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia mara baada ya kufungua mafunzo hayo.
************************
NAIBU Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewataka Wahifadhi kwenda kusimamia jukumu ya msingi la Wizara ya Maliasili na Utalii ambalo ni kulinda na kuhifadhi maliasili za Taifa ikiwemo Misitu na Wanyamapori
Mkomi ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 30, 2022 Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka
Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo yamehudhuriwa na Washiriki kutoka Jeshi la Polisi nchini , Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wahifadhi kutoka TANAPA, NCAA, TAWA na TFS,
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mkomi amesema Wahifadhi wana wajibu wa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama katika kuwabaini majangili wa wanyamapori na Misitu
Amewataka Washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo na kwenda kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha Wahalifu wa wanyamapori na misitu wanakamatwa kabla ya kuharibu Maliasili zetu.
“ Mafunzo hayo mtakayopewa yakawe chachu katika kuchagiza utalii hivi sasa filamu ya Royal Tour imeitangaza vizuri nchi yetu na Watalii wameanza kumiminika nchini kutokana na kazi kubwa mnayofanya ninyi Wahifadhi msingekuwa mmefanya kazi kubwa kulinda wanyamapori watalii wasingekuja kwa sababu kusingekuwa na wanyamapori ,” amesema.
Kutokana na jukumu walilonalo la kulinda Maliasili, Naibu Katibu Mkuu, Mkomi amewataka wahifadhi hao kuzingatia mafunzo hayo hususani suala la uchunguzi kwa kujifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha amesema suala la Uhifadhi linakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa Maliasili hivyo mafunzo hayo yakalete majawabu katika kulinda maliasili
Pia Dkt. Msuha amesema mafunzo hayo yanakwenda kuboresha utendaji kazi kwa kuhakikisha uhalifu wa wanyamapori na Misitu litachochea ufanisi zaidi katika utendaji w kazi wa kulinda maliasili zetu.
Naye Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Wanyamapori, Robert Mande amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa kukumbushana namna ya kushughulika na waharifu wa wanyamapori wa misitu mara wanapokamtwa.
“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona na waweze kuwa na usalama”Mande amefafanua.