**********************
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
IDARA ya afya Halmashauri ya Mji Kibaha,imejielekeza kupambana kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga ambapo kwa kipindi cha April hadi Juni mwaka huu 2022, vifo vya watoto wachanga 37 vimetokea hospital ya Rufaa Tumbi huku Kituo Cha afya Mkoani vifo vya watoto 13 .
Aidha mama wajawazito wamekemewa kuacha kutumia dawa za kienyeji kwa ajili ya kuongeza uchungu ili kuzaa haraka Jambo ambalo linasababisha madhara kwa mama mjamzito wakati wa kujifungua.
Akitoa ufafanuzi huo ,Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha,Dkt.Tulitweni Mwinuka alieleza , kwa kipindi cha January-March vifo vya watoto wachanga kwenye Kituo Cha afya Mkoani watoto 14 na hospitalini Tumbi January-March ni Jumla ya watoto wachanga 38 wamepoteza maisha .
“Mwaka 2022 January-March vituo vilivyopo Halmashauri na Tumbi hospital vimetokea vifo vinne vya uzazi na April -June vifo viwili ”
Alisema waliojifungua kawaida mwaka 2019 ni 8,213,mwaka 2020 ni 7,471 ,mwaka 2021 ni 8,244 huku upande wa upasuaji mwaka 2020 ni asilimia 18 na 2021 ni asilimia 20.
Tulitweni alieleza ,Mwaka 2019 katika Halmashauri na Hospital ya Tumbi vifo vya uzazi 26 watoto wachanga 146, mwaka 2020 wamama 11 na watoto wachanga 132 huku 2021 uzazi ni vifo Tisa na watoto wachanga ni 144.
“Hatuhitaji wala hakunaa anaependa kuona vifo vya uzazi na watoto wachanga,Tunapenda kuona vikipungua siku hadi siku ,Upande wa akinamama wajawazito na uzazi vifo vinapungua.”
Aliwataka , akinamama wajawazito kufika klinik mapema ili kupata elimu za uzazi,lishe na kupatiwa huduma bora hospital na kuepuka madhara yanayotokana na kuchelewa kuhudhuria klinik.
Mganga Mfawadhi Kituo Cha afya Mkoani,Dkt Godfrey Kajungu alisema ,wameboresha huduma ya wodi ya uzazi kwa kuweka upande wa Usiri kwa Gharama ya sh.milioni 12.2 kutoka ufadhili wa KOFIH.
“Wateja wanavutiwa na huduma hiyo wengi kwasasa wanakuja na ndugu zao ama mume ,na kuwa kwenye Mazingira ya usiri tofauti na zamani “alibainisha Kajungu.
Awali akizungumzia suala la vifo vya uzazi wakati wa Baraza la madiwani Mjini humo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mussa Ndomba aliiagiza idara hiyo kupeleka taarifa ya ukubwa wa changamoto zinazokabili kituo Cha afya Mkoani na hospital ya rufaa Tumbi ili kuona namna ya kusaidia.
Kuhusu Mapato ya Ndani ,Ndomba alisema wanashukuru Halmashauri hiyo imevuka Lengo kwa asilimia 105 la makusanyo kutoka Makadirio ya bil.4.9 hadi zaidi ya Bilioni 5.
Katika hatua nyingine, diwani viti maalum Kibaha Mjini ,Selina Wilson amechanguliwa Kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.