Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza na Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mhe. Macky Sall pembezoni mwa Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) unaoendelea katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Palais des Congres mjini Tunis,Tunisia, Agosti 28, 2022. Waziri Mkuu anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
KAMPUNI ya Japan ya Association of African Economic Development (AFRECO) imeonesha nia ya kujenga chuo cha uhandisi wa tiba (school of medical engineering) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ili kupunguza tatizo la wataalamu wa tiba na vifaatiba nchini.
Hayo yameelezwa na Rais wa kampuni hiyo, Bw. Tetsuro Yano jana jioni (Jumamosi, Agosti 27, 2022) alipokutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Tunis, Tunisia ambako anamwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD8).
Bw. Yano alisema walipokuja Tanzania waligundua kuwa kuna vifaa vinavyonunuliwa lakini vinashindwa kufanyiwa ukarabati pindi vikipata hitilafu sababu hakuna wataalamu. “Kwa kuzingatia hilo tumeona haja ya kuanzisha chuo cha uhandisi tiba ili tuweze kufundisha wataalamu watakaokuwa wakifanya matengenezo ya vifaa badala ya kuagiza mafundi kutoka nje, au kuviacha visitumike tena,” alisema.
Pia alimweleza Waziri Mkuu kwamba walishapokea maombi kutoka UDOM ya kupatiwa basi la kutoa tiba lenye vifaa mahsusi vya hospitali (mobile clinic bus) ambalo litakuwa likisaidia kutoa huduma kwenye vijiji vya jirani na chuo hicho.
Naye mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Sanaa cha Kurashiki cha Japan, Dkt. Tomotaka Naramura alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana nia ya kufungua chuo hicho mwaka 2023.
Alisema walikutana na Mkuu wa chuo hicho na wakakubaliana kuwa ipo haja ya kuendeleza rasilmali watu kwenye upande wa tiba ili kuwe na wataalamu mahsusi kwa ajili ya vifaa tiba vinavyonunuliwa.
“Tulikubaliana kwamba Tanzania ina vifaa tiba vya kisasa sana lakini kuna pengo la wataalamu wa kuviendesha na kuvifanyia ukarabati pindi vikipata hitilafu. Kwa hiyo tutatuma madaktari na mafundi kutoka Japan ili waje kuwafundisha vijana wa Kitanzania tuwe na kada ya wataalam ambayo kwa sasa ina uhaba mkubwa.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu aliwashukuru kwa kuonesha nia ya kuendeleza sekta ya afya na hasa kwenye eneo la vifaa tiba kwani linaendana na matarajio ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuboresha afya za Watanzania kwa kuhimiza ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati.
“Serikali ya Tanzania imeridhishwa na nia ya kampuni yenu ya kuwekeza kwenye uhandisi wa tiba kwani tunawahitaji sana watumishi wa hiyo kada. Hawa watasaidia siyo UDOM peke yake, bali Muhimbili, Bugando, KCMC na vituo vingi vya afya ambako Serikali ya awamu ya sita imepeleka vifaa tiba,” alisema.
Aliwataka waendelee kuwasiliana na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda ili kuhakikisha suala hilo linakamilika.