Na Mwandishi wetu, Mirerani
MCHIMBAJI wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Anselim Kawishe ametangazwa kuwa bilionea mpya wa madini ya Tanzanite.
Kawishe amekuwa bilionea mpya baada ya kupata vipande viwili vya madini hayo vya thamani ya sh2.2 bilioni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Nduguru amemtangaza bilionea huyo leo jumamosi Agosti 27 mji mdogo wa Mirerani.
Nduguru amemtangaza bilionea huyo mpya katika hafla ya ununuzi wa madini ya Tanzanite kuwa ni Anselim Kawishe.
Amesema Kawishe amepata vipande viwili vya madini ya Tanzanite vyenye uzito wa kilogramu 3.74 na kilogramu 1.48.
“Kati ya madini hayo mawili, yenye uzito wa kilogramu 1.48 ina thamani ya sh713.8 milioni na ya uzito wa kilogramu 3.74 yenye thamani ya sh1.5 bilioni jumla ni sh2.245 bilioni, amesema Nduguru.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amempongeza Kawishe kwa kufanikiwa kupata madini hayo.
“Hata mimi nisipokuwa bilionea, wananchi wangu wakiwa mabilionea ndiyo namimi nafarijika, tumezidi kuzalisha mabilionea wapya,” amesema Ole Sendeka.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite Sokota Mbuya amesema serikali inapoweka sheria rafiki za uchimbaji ndiyo sababu mabilionea wanazalishwa upya.