Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amewataka waandishi Halmashauri na Mkoa huo kufanya kazi ya usimamizi wa miradi ya ujenzi ili iwe bora na ikamilike ndani ya mkataba iliyowekwa.
Sendiga ametoa rai hiyo leo (26 Agosti,2022) alipofanya ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vituo vya afya na majengo ya shule wilayani Nkasi.
“Mhandishi wa sekretariati ya Mkoa na wenzako wa Halmashauri tokeni maofisini na kwenda maeneo ya miradi kusimamia kazi za ujenzi ili miundombinu hiyo ikamilike Kwa ubora na kuzingatia vigezo (BOQ) zilizopo” alisema Sendiga.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Mkoa alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Kasu kilichogharimu shilingi Milioni 500 lakini bado miundombinu yake haijakamilika huku ikihitaji fedha zaidi kukamilika.
Mradi wa pili aliokagua ni ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya kata ya Paramawe iliyopatiwa shilingi Milioni 470 ambapo ujenzi wake umefika asilimia 70 ambapo ameagiza apatiwe taarifa ya kina kwanini mradi huo haijakamilika na fedha zimeisha.Mradi huo ulitakuwa kukamilika Juni mwaka huu lakini sasa utakamilika Septemba30 mwaka huu.
“Tunataka kuona majengo yakiwa na ubora kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali hivyo sitaruhusu nyongeza ya muda au fedha bila kujua ukweli wa matumizi ya fedha zilizotolewa awali” alisisitiza Sendiga.
Tatu Mkuu huyo wa Mkoa alikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nkasi na kuagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa thamani ya fedha iliyotumika kwenye uagizaji na ununuzi wa vifaa vya ujenzi .
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Ibrahim Isaack alisema amepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kuwa miradi ya sekta ya Afya kuwa na uangalizi wa karibu ili ikamilike kwa wakati kote kwenye halmashauri Nne za Rukwa.
Dkt. Isaack alibainisha kuwa changamoto ya miradi mingi kutokamilika kwa wakati sasa inafanyiwa kazi huku akisema tatizo la uagizaji vifaa limechangia miradi kutokamilika kwa wakati.