*********************
NJOMBE
Mkazi wa kijiji cha Ilunda Bwana Seveline Kaduma aliyekuwa anagomea zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kile alichodai serikali imeshindwa kumtatulia migogoro yake ya tangu mwaka 2007 sasa amekubali kuhesabiwa baada ya mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony_mtaka kufika na kusikiliza kero zake.
Mkazi huyo bwana Kaduma anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 50 amesema mgogoro huo baina yake na ndugu zake waliokuwa wanamtishia maisha kwa kutaka kumpora mali za wazazi wake yakiwemo mashamba ameshindwa kutatuliwa na kukosa ushirikiano na ngazi mbalimbali za serikali licha ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka Amelazimika kufika kijijini hapo na kufanya mazungumzo naye yaliyomfanya kuridhia kuhesabiwa huku akitakiwa kufika ofisini kwake majira ya saa kumi jioni kwa mazungumzo zaidi huku akiwataka wananchi kutogomea zoezi la sensa kwa madai ya kutotatuliwa kero zao.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa ametoa onyo kwa wananchi ambao wanafanya ulimbukeni wa kujipiga picha zisizo na staha wakati wakihesabiwa na makarani na kuziweka mitandaoni.
Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za hadi usiku wa Agosti 25 mwaka huu mkoa wa Njombe umeshika nafasi ya pili kwa kutekeleza zoezi hilo vizuri ukiongozwa na mkoa wa Unguja kaskazini ambapo wakazi wa mkoa wa Njombe akiwemo Rosper Ndunguru,Elia Gadau na Gracious Chembela wamekiri kuhudumiwa vizuri na makarani wanaowafikia kwenye kaya zao huku makarani nao wakikiri kuonja joto la jiwe kwa mzee huyo kabla ya mkuu wa mkoa kufika kwenye kaya ya mzee Kaduma.