Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Kamati za Sensa za Mikoa kuhusu hali ya utekelezaji wa Sensa ya watu na Makazi kwa njia ya video, katika Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, Agosti 25 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*********************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa yote nchini waimarishe mawasiliano ili kutatua changamoto zitakazojitokeza wakati zoezi la sensa likiendelea.
Ametoa agizo hilo leo ( Alhamisi, Agosti 25, 2022) wakati akizungumza na wakuu wa mikoa kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya mtandao akiwa ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Kila siku saa 2 usiku kila mkoa uwe na takwimu za siku nzima. Hii itasaidia kubaini mapungufu yako wapi na kuongeza kasi kwenye maeneo ambayo yatabainika kuwa yanasuasua.”
“Kamati za Sensa za mikoa na wilaya nazo pia ziwe barabarani ili kufuatilia mwenendo wa sensa katika maeneo yao. Hii itawapa uhakika makarani wetu wakijua kuwa mnawafuatilia.”
Pia, Waziri Mkuu amesema ipo haja ya kudhibiti tabia ya upotoshaji inayofanywa kwenye mitandao ya jamii. “Zungumzeni na watu wenu wa TEHAMA ili wafuatilie. Pia picha zenye matumizi ya reflectors yasiyokuwa sahihi, ziachwe kusambazwa.”
Amesema wakuu wa mikoa kwa kushirikiana na Kamati za Sensa wahakikishe maeneo yote yanafikiwa, kaya zote zinafikiwa na watu wote wanahesabiwa.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema hadi kufikia tarehe 25 Agosti, 2022 kaya 5,060,158 zilikuwa zimeshahesabiwa nchi nzima sawa na idadi ya watu 22,004,910, kati ya hao wanawake 11,413,045 (51.9%) na wanaume 10,591,865 (48.1%).
“Uchambuzi unaonesha kuwa mikoa yote 36 imeweza kuhesabu watu kwa wastani wa asilimia 36.8. Mkoa unaoongoza kwa kasi kubwa ni Kaskazini Unguja ambapo asilimia 49.7 ya kaya zote zimeshahesabiwa.”