Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
VIKUNDI vya kijamii Wilayani Kibaha, vimetakiwa kutenga mafungu ya fedha kwa ajili ya kusaidia watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu ikiwa ni sehemu ya kujitolea kwenye jamii.
Katibu wa kikundi cha Super Women 2017 cha Mkuza, Maria Msimbe alitoa wito huo wakati walipokwenda kutoa msaada wa vyakula mbalimbali, kwenye kituo cha watoto waishio kwenye mazingira magumu cha Buloma kilichopo Sofu.
Msimbe alieleza, kikundi hicho kinasaidiana na kukopeshana fedha na kimeamua kutoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya mapato yao.
“Fedha tulizonunulia vyakula hivi zinatokana na mfuko wa jamii ambao ni sehemu ya michango ya wanachama na fedha hizo hutumika kwa ajili ya matendo ya huruma kama hili,”alisema Msimbe.
Alisema, vikundi vingine vya kijamii vinapaswa kuwa na fungu maalumu kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji kama hawa .
“Jamii zenye uhitaji zinatutegemea sisi hivyo wanajamii tuungane kuwasaidia kwani kutoa ni moyo”alisema Msimbe.
Naye Mlezi wa kikundi hicho ,Beth Msimbe alifafanua, anasimamia kuhakikisha kikundi hicho kinawakwamua mabinti kutokana na changamoto mbalimbali za kimaisha na kuwapa ujasiri waweze kupambana kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Msaidizi wa kituo hicho Baraka Peter alieleza, wanajiendesha na kutegemea wadau,wana miradi ya duka, uuzaji wa mafuta ya alizeti na maziwa ya ng’ombe ,Kituo kimeanza ujenzi wa shule ya awali ya kutwa ambayo imefikia hatua ya linta na kina watoto 42.