Na Dotto Mwaibale, Singida
SHEIKH wa Mkoa wa Singida,Issa Nassoro
amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu mkoani hapa kuendelea kuwahamasisha
waislam kwa kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa ya Watu na Makazi
wanaopita kwenye majumba yao kwa ajili ya kuwahesabu.
Nassoro alitoa wito huo jana baada ya kuhesabiwa na familia yake nyumbani
kwake eneo la Manguanjuki lililopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida ambapo alisema kuwa sensa
katika Uislamu inakubalika na ilianzishwa na Mtume Muhammad (SAW) na kuwa kama
kutatokea watu wakiipinga wanapaswa kupewe elimu.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba Waislam wote mkoani hapa waendelee kutoa
ushirikiano kwa makarani wanaofanya zoezi
la sensa ya watu na makazi ambayo ni muhimu sana kwa kila mwanananchi na
taifa kwa ujumla” alisema Nassoro.
Sheikh Nassoro alisema baada ya kumalizika kwa sensa hii ya kitaifa waislam
wote wa Mkoa wa Singida watafanya sensa yao ili kupata idadi yao kwa ajili ya
kusaidia kupanga mipango yao ya maendelea ikiwemo ya kujenga, shule, madrasa na
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa .
“Tutafanya sensa yetu ya kiislam ili tuweze kufahamiana na kuhimizana
kufanya michango kwa ajili ya maendeleo mbalimbali hatuwezi kushindwa nitolee mfano kwa waislam
4000 kila mmoja akiamua kuchangia Sh.5000 tu kwa mwezi tutakuwa tumepata fedha
za kuanza kujenga hospitali yetu”alisema Sheikh Nassoro.
Aliongeza kuwa , sensa ni jambo jema lenye maana, na katika Uislamu hakuna
mahala ambapo hawajazungumza habari za sensa, hata katika vitabu vingine
tumesoma vimezungumza habari hizi. Hata Mtume alitumia sensa kujua jeshi lake
lina watu wangapi.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Singida, Ahmed Kaburu Akizungumzia
Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 baada ya kuhesabiwa pamoja na
familia yake alisema ni kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi
zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025,
mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za
maendeleo za kimataifa.
Alisema taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika
utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi
husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali na kupata taarifa za
msingi za hali ya kidemografia, kijamii na kiuchumi za idadi ya watu na makazi
za mipango katika ngazi zote.
Aidha Kaburu alisema umuhimu wa sensa hiyo ni pamoja na kigawio katika
kukokotoa viashiria vingine mfano Pato la mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa, Ajira
na ukosefu wa Ajira na kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi.
Pia alisema umuhimu wa sensa hiyo ni kupata taarifa itakayowezesha serikali
kujua ongezeko la idadi ya watu, kwa mgawanyo na viashiria vingine, ambavyo ni
muhimu kwa usimamizi wa mazingira na msingi wa utawala bora na ujumuishaji wa
demokrasia.