Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Karani wa Sensa Phausta Ntigiti wakati alipokuwa akihesabiwa katika Makazi yake Chamwino Ikulu Mkoani Dodoma tarehe 23 Agosti, 2022 kwenye shughuli ya Sensa ya Watu na Makazi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuhesabiwa katika Makazi yake Chamwino Ikulu Mkoani Dodoma tarehe 23 Agosti, 2022 katika shughuli ya Sensa ya Watu na Makazi.
KAMISAA wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania bara Anna Makinda,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhesabiwa katika Makazi yake Chamwino Ikulu Mkoani Dodoma tarehe 23 Agosti, 2022 katika shughuli ya Sensa ya Watu na Makazi.
…………………………..
Na Alex Sonna-CHAMWINO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,amewaongoza watanzania kuhesabiwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi huku akiwataka wananchi kuandaa mapema majibu ya maswali yaliyoko kwenye dodoso ili kuwarahisishia kazi makarani.
Rais Samia amehesabiwa leo Agosti 23,2022 na Karani Phauster Ntigiti kwa takribani dakika 30 kwenye makazi yake Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhesabiwa Rais Samia Suluhu Hassan amewashauri viongozi wa kaya kuhakikisha wananchi wanaandaa mapema viambatanisho kamili nyumbani ili makarani wanapopita wafanye kazi kwa urahisi na kwa muda mfupi.
“Watanzania wenzangu zoezi hili ni la kawaida sana Mimi tayari nimehesabiwa pamoja na familia yangu,muhimu tu ni kuandaa vitambulisho vyote ili kuwa navyo karibu karani akifika usipate usumbufu wa kuanza kutafuta viko wapi,ukiviandaa zoezi haliwezi chukua muda mrefu,”almesema Rais Samia.
Hata hivyo amewataka Makarani kufanya kazi zao kwa ufanisi na wananchi watoe majawabu yanayotakiwa ili kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu, Anne Makinda,amesema kuwa Sensa hiyo itafanyika kwa siku saba na kuwaomba wananchi wawe wavumilivu.
“Tunawaomba wananchi wasituchoke sisi Maafisa Zoezi hili Leo mpaka tukikamilisha itakuwa ni asilimia 15 na hili zoezi litakuwa kwa muda wa siku saba tunaomba utulivu na uvumilivu”.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dokta.Albina Chuwa amesema hadi kufikia saa 5 asubuhi kaya elfu 7,768 nchi nzima zimehesabiwa na makarani nchi ikiwemo waliolala kwenye nyumba za wageni na wasafiri.
Dokta Chuwa ameyasema hayo leo alipokuwa akikagua kituo cha upokeaji taarifa za sensa ya watu na makazi(Data center) kilichopo Njedengwa Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC.