Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Katibu wa Taasisi ya Jamii Mpya mkoa wa Pwani kupitia kampeni ya MAMA YANGU NCHI YANGU, Rehema Kawambwa ametoa Rai kwa jamii ,kujenga tabia ya kutembelea vivutio na kufanya utalii wa ndani ili kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia kutangaza na kupenda utalii wa kwetu.
Aliyasema hayo Bagamoyo,baada ya baadhi ya wanachama wa jamii mpya Pwani ,kwenda kutembelea vivutio wilayani humo na kutumia fursa hiyo kuhamasisha wavuvi ,vijana , wajasiriamali na wananchi kijumla kujitokeza katika Zoezi la sensa .
Rehema alisema ni wakati wa kuendelea kumuunga mkono Rais wetu kutalii na kujionea vivutio vyetu pasipo kusubiria kuhadithiwa.
“Utalii unaongezea pato Taifa lakini pia unasaidia kutalii, kujua historia ya vya kwetu na kujiliwaza “alifafanua.
Rehema alimshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuionyesha dunia kuwa wilaya ya Bagamoyo ambayo ipo Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa wilaya zenye vivutio vikubwa vya utalii katika Tanzania.
Alisema kitendo cha Rais Samia kufika Bagamoyo katika maandalizi na utengenezaji wa filamu ya ‘’Royal Tour’’ na kisha kutangazwa kwenye filamu hiyo ni kielelezo tosha kuwa Bagamoyo ni kitovu cha utalii .
“Tunashuhudia sasa baada ya Rais kuvalia njuga suala la utalii na kutangaza vivutio vilivyopo nchini sasa watalii wanamiminika na wawekezaji wanaongezeka,ni suala la kumshukuru kwani tunaendelea kuongeza Pato la nchi kwa kodi na kuinua uchumi”
“Pia napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Ndg. Shauri Selenda, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mhe. Muharami Mkenge, Ofisi ya Kata ya Dunda, pamoja na Viongozi wa Jamii Mpya Wilaya ya Bagamoyo Mama Shumina Rashid, Ester Lumato na Hanipha Checheta kwa mapokezi mazuri.”
Aidha, napenda kuwashukuru Twiga Entertainment na wote walioshiriki nasi katika MATEMBEZI YA HAMASA YA SENSA NA UTALII – BAGAMOYO, yaliyoandaliwa kwa ajili ya kuwahamasisha watu kushiriki kwenye zoezi la kuhesabiwa katika Sensa ya watu na makazi (23/08/2022).