*************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Hassan Serera, amehitimisha Sensa Cup Bonanza kwa kuipatia timu ya Tanzanite Sports Academy kombe na mpira mmoja kwa kutwaa ubingwa huo.
Bonanza hilo limeshirikisha timu sita na kufanyika kwenye viwanja vya Tanzanite Complex Stadium Mji mdogo wa Mirerani.
DC Serera ameikabidhi mipira miwili kwa timu ya Naisinyai FC kwa kuwa washindi wa pili na timu ya watumishi FC ikapata mipira mmoja kwa kushika nafasi ya tatu.
“Bonanza hili limefanyika ili kuhamasisha Sensa ya watu na makazi Agosti 23 ila mnapaswa kutambua kupitia michezo vijana wanapata ajira na kujenga afya zao kwani michezo ni furaha na mshikamano,” amesema DC Serera.
Mwenyekiti wa chama cha soka Wilaya ya Simanjiro Charles Mnyalu amempongeza DC Serera kwa kufanikisha bonanza hilo kwani vijana wameonyesha vipaji vyao.
“Pamoja na hayo tuna timu yetu ya wasichana ya Tanzanite Queens tunaomba utuunge mkono ili tufike mbali zaidi kwani wadada hawa wana vipaji vikubwa,” amesema Mnyalu.