Adeladius Makwega–DODOMA
Ili mtu aweze kufanya uhalifu wowote ule kwanza ni lazima mtu huyo awe na nia ya kulifanya jambo hilo ovu. Pili, akishapata nia au kusudio la kulifanya jambo hilo ndugu huyo atapata au kutafuta pahala/ sehemu/ eneo la kufanya uovu huo. Tatu, akipatambua pahala hapo ndugu huyu atajiuliza swali, je huo uovu ataufanya yeye mwenyewe au kwa shirika?. Nne, akishatambua hilo anaweza kuufanya uovu huo kwa kutumia mwili au kwa kutumia silaha yoyote ile?(atafanyaje huo uhalifu?). Tano, mhalifu huyo tarajali sasa atafanya uhalifu huo baada ya kuwa na majibu hayo ya masuala yote matano ili kuikamilisha nia yake ovu.
Kwa kutazama maswali hayo natumia herufi P kuyatambulisha na kuyaita P1, P2, P3, P4 na P5. Sasa, hili kuweza kuzuia uhalifu kama wa wizi au uhalifu mwingine kuna mbinu tofauti za kuzuia kwenye hatua za mwanzo.
Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Augustino Lyatonga Mrema ambaye amefariki dunia ambayo aliiongoza tangu mwaka 1991-1994 alifanya kazi nzuri sana akiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo Haruni Mahundi ambaye alikuwa IGP tangu 1984-1996.
Mheshimiwa Mrema alikuwa na dhana ya kupambana na uhalifu katika hatua za awali kama nilivyozitaja hapo juu.
Jambo hili kwa hakika lilisaidia mno kupunguza uhalifu hasa hasa kwa kutumia polisi jamiii iliyokuwepo nchi nzima kwa kila mtu kulilinda eneo lake.
Enzi za Waziri Mrema mhalifu huyo anapokuwa na nia ovu pale anapotaka kwenda kuufanya uhalifu huo tu pale pale akitoka katika nyumba yake alikutana na sungusungu na maswali yalikuwa mengi, wewe ni nani? Unakwenda wapi? Umebeba nini? Au wale waliokwisha fanya uhalifu unatoka wapi na umebeba nini? Mrema aliuzuia uhalifu katika hatua za mwanzo yaani P1, P2, P3 au P4.
Kama uhalifu wa wakati huo ukifikia hatua ya P5 hapo utakuwa umewahusisha watu wengi sana na jambo hilo lilifanya kuweza kujulikana na polisi nao kudhibiti uhalifu huo kwa uwezo na nguvu zote.
Unaweza kuzuia uhalifu katika hatua ya P1 na P2 kwa kuangalia kipi kinasababisha mtu huyo kujihusisha katika uhalifu huo? Kwa mfano umasikini, japokuwa watu wengine ni wahalifu kwa tabia tu. Kama umasikini ni kisababisho kinaweza kutatuliwa hasa kwa kutoa ajira kwa jamii hiyo.
Ulinzi wa sungusungu uliratibiwa na wajumbe wa nyumba kumi kumi na wajumbe hao walitambua hata tabia za watu wote waliokuwa wakiwaongoza. Kwa mfano katika nyumba moja hadi nyingine kila mmoja alijulikana kwa jina na tabia yake iwe njema au mbaya. Sungusungu wa enzi za Mrema waliweza kusaidiana kwa karibu sana na polisi waliokuwepo katika Vituo Vidogo ambavyo venyewe vilikuwa jirani na makaazi ya raia. Vituo hivyo vidogo kama walishindwa kupambana na uhalifu huo walisaidiwa sana na Vituo Vikubwa vya Polisi huku kukiwa na magari za polisi yaliyokuwa yakifanya dolia.
“Nakumbuka mtaani kwetu palikuwa na Stafu Sanjenti Msaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) , akiwa ni mjumbe wetu wa nyumba kumi kumi akifahamika kama Omari Idi Waziri, yeye ndiye alikuwa akisimamia zoezi hilo, nao wana mtaa wakichanga fedha za betri za tochi hizo.”
Japokuwa binafsi sikushiriki ulinzi huo kwa kuwa nilikuwa mwanafunzi, lakini nilimsikia fika Stafu Sajenti Waziri (mstaafu) akisema kuwa Waziri Mrema alikuwa akikagua mitaani zoezi hilo la ulinzi wa sungusungu.Kama Mrema alikagua kweli au la, zoezi hilo mawazo hayo yalisaidia mno kulipa nguvu kubwa zoezi hili.
Ujenzi wa vituo vidogo vya polisi ulikuwa unafanywa na wananchi wenyewe kwa kujichangisha na ujenzi huu ulifanyika kama ujenzi wa shule ya sekondari za kata. Kwa hiyo hapo serikali ilikuwa ikitoa ramani tu na wananchi walijenga chini ya usimamizi wa serikali za mitaa au vijiji na kweli mara vilipomalizika Mheshimiwa Augustino Mrema alifika kuvifungua na kumuagiza RPC wa eneo hilo kupeleka askari polisi na muda mwingine polisi walipelekwa katika vituo hivyo hata kabla mheshimiwa Mrema hajavifungua.
Hoja ya sungusungu na vituo vidogo vya polisi zilikumbwa na upinzani mkubwa kwanza wakisema kuwa sungusungu hawakuwa na ujuzi wa kupambana na wahalifu na polisi ndiyo wenye ujuzi huo wa kupambana na uhalifu. Hoja hii ya kupinga ulinzi wa sungusungu ilipata nguvu zaidi baada ya Mrema kutoka katika Baraza la Mawaziri na baadaye kuondoka upinzani, ikionekana kama ni hoja binafsi ya Mrema.
Wazo la Mrema halikuwa sungusungu kupambana na wahalifu katika ngazi ya silaha tu bali kufanya mapambano ya uhalifu katika ngazi za awali kama nilivyodokeza hapo juu P1, P2, na P3.
Japokuwa polisi wamejifunza kupamba na uhalifu, swali ni je wananchi wabweteke na kuwaacha wahalifu kuwasubiri polisi waje kupambana nao? La hasha nia ya Mrema ilikuwa kila mmoja wetu awe mlinzi wa raia wenzake na mali zao pahala alipo.
Ifahamike wazi polisi ni binadamu kama mimi na wewe, wenye damu, nyama na mifupa na panapotokea matukio ya uhalifu mkubwa huwa wanapata madhara na hata kupoteza maisha. Hakuna mwenye mwili wa chuma. Ndiyo kusema ulinzi ni ushirikiano kwa raia wote.
Ukija katika dhana ya pili ya Mrema ya ujenzi wa vituo vidogo vya polisi ambao kwa sasa haupigiwi chapuo sana, kumekuwa madai kuwa wananchi walishiriki kwa sehemu kubwa kutoa fedha na rasimali zao. Wapo wanaodai kuwa baadhi ya watendaji ndani ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi yetu wakati huo, ujenzi wa vituo vidogo waliliona zoezi hili kuwa kama vituo hivyo vingejengwa kwa kasi sana bajeti ya Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi ingepungua na kupunguza kasi ya ujenzi wa vituo vikubwa vya Polisi.
Hoja za kuwa vituo vidogo vinaweza kuvamiwa na wahalifu ikashika kasi, huku kukitolewa mfano wa matukio hayo ya uvamizi wa vituo vidogo na kweli kasi ya ujenzi wa vituo vidogo ikazikwa katika kaburi la sahau.
Binafsi nasema wazi kuwa ujenzi wa Vituo Vidogo vya Polisi kama ukiendelezwa unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa kumlinda raia na mali zake huku Serikali kuu ikiendeleza ujenzi wa Vituo Vikubwa vya Polisi.
Wananchi wanaposhiriki kujenga vituo vidogo vya polisi wataona kuwa ni vituo hivi ni mali yao na polisi ni ndugu zao na hata kuongeza ushirikiano kwa zaidi na zaidi na jeshi hili.
Mzee wetu marehemu Augustino Lyatonga Mrema alifanya kazi kubwa sana kwa Watanzania lakini alihitilafiana na wanasiasa wenzake aliokuwa nao CCM wakati huo. Je kuhitilafiana huko kunaweza kufuta uhodari wake aliyofanya kwa Watanzania akiwa kiongozi wa serikali? Binafsi ninaimani kuwa mema aliyoyatenda kwa taifa hili hayajaandikwa wa kalamu ya risasi kwamba yanaweza kufutwa kwa sekunde moja, abadani. Ukitaka kuyafuta mema ya Mrema basi jiandae kuiondoa hata karatasi iliyotumika kuandikia mema hayo na hilo haliwezekani.
Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazia, apumzike kwa amani amina.