Na. Damian Kunambi, Njombe
Serikali kupitia naibu waziri wa madini Steven Kiruswa imeunda timu ya wataalam itakayofanya kazi ya kuchambua reseni zote za miradi ya makaa ya mawe wilayani Ludewa mkoani Njombe zilizotolewa na kisha kutoa mapendekezo juu ya wachimbaji wadogo wakiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa pamoja na chama cha mapinduzi ili waweze kupewa maeneo ambayo hatatumia gharama kubwa ya uchimbaji.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao cha baraza la madiwani mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema kamati hiyo inahusisha MMI, NDC, mwanasheria wa Halmashauri, Afisa tarafa ya Mawengi pamoja na katibu wa mbunge ambayo imepewa majuma matano ya kushughulikia zoezi hilo na kutoa majibu.
Ameongeza kuwa kwa muda mrefu baraza hilo lilikuwa likitoa mapendekezo hayo ya ugawaji vitalu kwa wachimbaji wadogo kwakuwa maeneo hayo hayaja endelezwa kwa muda mrefu hivyo kwa hatua hiyo iliyofikiwa ni fursa ya kipekee ambayo inaenda kutimiza ndoto ya baraza hilo.
Aidha kwa upande wa mwenyekiti wa Halmashauri Wise Mgina amempongeza mbunge kwa ufuatiliaji wake wa jambo hilo kwani endapo watagawiwa vitalu hivyo itasaidia kukuza uchumi wa Halmashauri na kuleta mzunguko mkubwa wa fedha kwa wilaya ya Ludewa.
“Halmashauri yetu ina miradi mingi ambayo ikifanyiwa kazi itakuza uchumi wetu, kila wakati baraza linapokutana tumekuwa tukiimba wimbo huu wa wachimbaji wadogo kupewa vitalu hivyo tunashukuru kwa walio tuwakilisha katika makubaliano hayo kwani mmefanya makubaliano yenye tija kwa halmashauri yetu”, Amesema Mgina.