*****************************
Na Mwandishi Wetu, Babati
UTALII wa picha unaofanywa na Kampuni ya EBN Hunting Safari umewezesha wanyama katika eneo la Jumuiya ya Wahifadhi Wanyamapori (WMA) Buringe wilayani Babati mkoani Manyara kuongezeka kwa asilimia 85.
Hayo yamesemwa na Ofisa Mawasiliano wa EBN Charles Sylvester wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea katika kitalu cha WMA Buringe.
Charles alisema awali kitalu hicho kilikuwa kinafanya utalii wa uwindaji hali ambayo ilisababisha wanyama kuhama ila baada ya wao kuanza kutoa huduma ya utalii wa picha wanyama wameongeza kwa wingi.
Alisema wanyama wengi wanapenda maeneio ambayo ni tulivu hivyo EBN imeamua kusimamia mfumo huo ambapo matokeo yameonekana kuwa mazuri.
“Tumekuwa tukifanya utalii wa picha katika kitalu hiki ambapo matokeo yameonekana kuwa makubwa kwa wanavijiji kunufaika, ila kubwa zaidi ni wanyama kuongezeka kila siku,” alisema.
Ofisa huyo alisema utalii wa picha unavutia wanyama kwa kuwa kuna utulivu mkubwa tofauti na awali ambapo milio ya bunduki ilikuwa inasikika hivyo kuwakumbiaza.
Alisema kupitia utalii huo pia wameweza kufanikisha ongezeko la watalii kutoka nchi mbalimbali hali ambayo inaongeza mapato kwenye WMA na wawekezaji.
Sylvester alisema uwekezaji huo umefanikisha kutoa ajira zaidi ya 50 kwa vijana wa Kitanzania ambao wanahudumia watalii na kulinda wanyama wasidhuriwe.
“Utalii wa picha ambao unafanyika hapa Buringe unalipa, kwani mtalii akija anapiga picha anaondoka na mnyama anabaki, hivyo tunashauri wawekezaji wengine kuwekeza katika utalii huu,” alisema.
Alisema pamoja na kuwepo na mafanikio katika utalii huo wa picha zipo changamoto za mifugo kuingia ndani ya hifadhi, hivyo kutoa rai kwa wafugaji kuzuia mifugo yao.
Aidha ofisa huyo alisema kwa miaka takribani tisa ya uwepo wa EBN katika eneo la Buringe umefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande Mhifadhi wa Wanyamapori Wilaya ya Babati, Samuel Bayo alisema ujio wa EBN umekuwa na faida nyingi, ila kubwa ni kuongezeka kwa wanyama na utulivu kuongezeka.
Alisema pia uwekezaji huo wa utalii wa picha umepunguza hali ya ujangili ambao ilikuwa imezoeleka kwa miaka mingi.
“Sisi kama Serikali tunashirikiana na watu wa EBN, na Buringe WMA kuhakikisha ulinzi wa wanyama unakuwepo na hili limefanikiwa ndio maana unaona tembo wapo wengi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazato Twange alisema WMA zilizokuwepo katika wilaya hiyo zimekuwa ni chanzo muhimu kwa mapato ya Serikali, hivyo watahakikisha zinaendelea.
Twange alisema wanatarajia kuanzisha WMA zingine katika maeneo ambayo yana sifa ya kufanya hivyo ili kuhakikisha uhifadhi unaongezeka na kuongeza mapato.