Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Mbinga George Mhina kulia,akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kituo cha afya Matiri kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas katikati aliyetembelea mradi huo kwa ajili kuweka jiwe la msingi,kushoto Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosono.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Juma Haji kulia,akimuongoza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas katikati kukagua majengo ya kituo cha afya Matiri kinachojengwa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kwa gharama ya Sh.milioni 500 ili kuwapunguzia kero ya kwenda umbali mrefu wakazi wa kata ya Matiri kwenda maeneo mengine kufuata huduma za afya,kushoto Mkuu wa wilaya hiyo Aziza Mangosongo
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kulia,akikagua maeneo mbalimbali ya ujenzi wa mradi wa kituo cha afya Matiri kinachojengwa na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo,katikati ni Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo George Mhina.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas, akiondoa kitambaa wakati wa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya Matiri Halmashauri ya wilaya Mbinga,kulia mkuu wa wilaya hiyo Aziza Mangosongo na wa kwanza kushoto Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Juma Haji.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini Benaya Kapinga kushoto,akiteta jambo na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas wakati wa uwekezaji jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya Matiri wilayani humo Mbinga.
Baadhi ya wazee wa kijiji cha Matiri kata ya Matiri wilayani Mbinga,wakimpa zawadi ya Mbuzi Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas baada ya Mkuu wa mkoa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa kituo cha afya matiri.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas kulia,akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo baada ya kukagua kituo cha afya Matiri pamoja na kuzungumza na wakazi wa kata hiyo.
Picha na Muhidin Amri,
……………………………………..
Na Muhidin Amri,
Mbinga
WAKAZI 13,000 wa kata ya Matiri Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wanatarajiwa kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya matibabu baada ya Halmashauri ya wilaya kuanza ujenzi wa kituo cha afya katika kijiji cha Matiri.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbinga Juma Haji kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas,Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo George Mhina alisema,lengo la kujenga kituo hicho ni kuboresha huduma za afya ya jamii na kuleta ukombozi kwa wananchi.
Alisema,kazi za ujenzi ikiwamo kusafisha eneo la ujenzi kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo zilianza mwezi Februari mwaka huu na zilitarajiwa kukamilika tarehe 30 ,lakini kutokana na changamoto ya hali ya hewa wanatarajia kukamilisha mradi huo mwezi Septemba.
Kwa mujibu wa Mhina,kazi ya ujenzi wa mradi huo zinaendelea vizuri ambapo hadi sasa hatua iliyofikiwa inaridhisha kwani jengo la wagonjwa wa nje(OPD) na maabara yako katika hatua ya kupaka rangi.
Alitaja, kazi nyingine zinazoendelea ni jengo la upasuaji,jengo la mama na mtoto na jengo la kufulia nguo ambayo yapo katika hatua ya kupiga lipu na mategemeo katika awamu ya pili jengo la mama na mtoto na jengo la kufulia nguo yatakamilika katika kipindi cha miezi mitatu.
Mhina ambaye ni Katibu wa afya wa Halmashauri ya wilaya alieleza kuwa,mradi hadi utakapokamilika utagharimu jumla ya Sh.milioni 500 zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya na mchango wa wananchi ni Sh.milioni 11 na hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh.milioni 379.
Mhina alisema, malengo ya Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo ni kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati kwa kuzingatia uwajibikaji na kuweka maslahi ya mradi mbele.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kazi nzuri ya kusimamia makusanyo ya ndani na kutekeleza vyema miradi mbalimbali inayolenga kuchochea maendeleo kwa wananchi.
Alisema,Halmashauri zikikusanya vizuri mapato yake zitakuwa na uwezo wa kujiendesha na kutekeleza mipango iliyojiwekea badala ya kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu au kwa wahisani.
Kanali Laban amezitaka Halmashauri nyingine katika mkoa huo kuiga mfano wa Halmashauri ya Mbinga katika ukusanyaji madhubuti wa mapato ya ndani na kutekeleza miradi ya mbalimbali ya maendeleo pasipo kusubiri msaada kutoka kwa watu wengine.
Kanali Laban,amewapongeza wananchi wa kata ya Matiri kwa kuchangia fedha zaidi ya Sh.milioni 11 katika ujenzi wa mradi huo na kuwataka kushirikiana na Halmashauri yao ili kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Katika hatua nyingine,mkuu wa mkoa amewaomba wananchi wa wilaya ya Mbinga kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 23 mwezi huu kwa ajili ya kushiriki zoezi la sense ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Alisema,zoezi la sensa ya watu na makazi ni muhimu sana kwa maendeleo na uchumi wa nchi yetu kwani inatoa nafasi kwa serikali kutambua idadi ya watu wake na kamwe zoezi hilo halihusiani na itikadi za vyama vya siasa.
“ndugu zangu wa Mbinga kama tutafanya kosa mwaka la kutojitokeza kwa wingi kuhesabiwa basi tutafanya kosa kubwa ambalo litasababisha kukosa taarifa na takwimu sahihi za watu wake”alisema.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga vijijini Benaya Kapinga ameipongeza Halmashauri kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha huduma za afya,ambapo kwa mwaka 2022 inajenga vituo vitatu vya afya vya Matiri,Muungano na Mkumbi.