Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV-Uyui
KATIBU wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka amemshauri Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff kuwasimia vema mameneja wa Wakala huo wilaya na mikoa ili kuhakikisha wakandarasi wababaishaji na walioonesha uwezo mdogo kwenye utekelezaji wa miradi ya barabara wanasitishiwa mikataba na kutokupewa kazi za TARURA nchi nzima.
Shaka ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa kata ya Igulungu, Jimbo la Tabora Kaskazini baada ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Gilimba katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora ambayo ipo katika hatua ya ukamilishaji.
Shaka aliyasema hayo baada ya wananchi kulalamikia ubovu wa barabara yao ya Igulungu ambayo ina mkandarasi anaijenga na amelipwa kiasi cha Sh.milioni 60 kati ya Sh.milioni 499 za mradi huo lakini kazi inasuasua na hata maeneo aliyoyajenga yapo chini ya kiwango.
“Inasikitisha TARURA mnakiri hapa kuwa mmepokea fedha Sh.milioni 499 na mkasaini mkataba na mkandarasi mwezi Juni 2021 ambao alipaswa kuikamilisha kazi ndani ya miezi sita, leo ni mwezi Agosti, 2022 miezi 14 tangu mpokee fedha na kumpata mkandarasi bila kazi kukamilika. Wawakilishi wa wananchi wamelalamika mkandarasi hana uwezo na ninyi TARURA mmekiri hilo ila mnafikiria kuvunja mkataba wake mpaka sasa.
“Ushauri Wangu vunjeni mkataba na mkandarasi huyo na wengine wote ambao hawafanyi vizuri ili wapewe kazi wakandarasi ambao wanauwezo wa kufanya kazi kwa viwango na kasi inayotakiwa.
“Serikali ya CCM Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inataka kupeleka huduma kwa wananchi kwa kuboresha mawasiliano ya miundombinu ya barabara hasa vijijini ndio maana imeiimarisha sana TARURA kwa kuiongezea fedha kutoka Sh.bilioni 276 hadi Sh. bilioni 750 katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Jimbo hili lilipata Sh. bilioni 1.5. Ongezeko hili ni ili TARURA iweze kuwahudumia watanzania kikamilifu katika miundombinu hii ya barabara.” Amesema Shaka
Shaka amesisitiza lengo la kuanzishwa kwa TARURA nchini ni kuhakikisha inawasaidia wananchi katika Suala zima la ujenzi wa miundombinu ya barabara ili kuwarahisisha katika usafirishaji wa mazao, bidhaa na kwenye kufuata huduma za kijamii. Hivyo ni muhimu kutumia wakandarasi wenye sifa na uwezo wa kufanya kazi ili kuhakikisha miradi wanayopatiwa na Serikali inakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya CCM ya Umoja wa Wazazi Tanzania Ndg Gilbert Kalima ambaye ameambatana na Shaka katika ziara hiyo amewataka wananchi kujitokeza kuhesabiwa siku ya sensa Agosti 23, 2022.
‘CCM Imara, Shiriki Uchaguzi Kwa Uadilifu na Jiandae Kuhesabiwa Agosti 23, 2022.’
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa Itikadi na Uenezi Ndg Shaka Hamdu Shaka akizungumza na mbele ya akizungumza na wanachama
wa CCM na wananchi wa kata ya Igulungu, Jimbo la Tabora Kaskazini baada
ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Gilimba katika Halmashauri
ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora ambayo ipo katika hatua ya
ukamilishaji,pichani kulia ni Meneja wa TARURA wilaya ya Uyui Rahab Thomas
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa Itikadi na UeneziShaka Hamdu Shaka(kushoto) akimsikiliza Meneja wa TARURA wilaya ya Uyui mkoani Tabora Rahab Thomas alipokuwa akieleza changamoto zilizopo kwenye mradi wa barabara ya Igulungu wilayani humo.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka akipokelewa a na Wana CCM pamoja na wananchi wa Kata ya Igulungu , Jimbo la Tabora Kaskazini baada
ya kufika kwenye kata hiyo kwa ajili ya kukagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Gilimba katika Halmashauri
ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora .