Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya muendelezo wa kuripoti habari za Sensa kwa waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa chama cha kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu nchini (OJADACT) Edwin Soko akizungumza kwenye mafunzo ya muendelezo wa kuripoti habari za Sensa kwa waandishi wa habari
Lucyphine Kilanga mratibu wa OJADACT akitoa mada ya maana ya Sensa na umuhimu wake katika kuleta maendeleo kwenye mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari .
Baadhi ya Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali Kanda ya ziwa,uongozi wa chama cha kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu nchini (OJADACT) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mwenye Tisheti nyeupe mara baada ya kufungua mafunzo
……………………………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
CHAMA cha kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu nchini (OJADACT) kimeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari wa Kanda ya ziwa kwa lengo la kuwapa elimu ya umuhimu wa kuendelea kuandika habari zinazohusu sensa.
Mafunzo hayo ya siku moja yamehudhuliwa na waandishi wa habari zaidi ya 20 yamefanyika leo Agositi 20,2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana
Mwenyekiti wa OJADACT Edwin Soko, amesema wameandaa mafunzo hayo kwa lengo la kuwafundisha waandishi wa habari namna ya kuendelea kuandika habari za Sensa ili jamii iendelee kufahamu kwamba baada ya Sensa mabadiliko gani yamepatikana.
Soko amewaasa waandishi wa habari kuwa mabalozi wazuri kwenye Sensa ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika kuielimisha jamii kujitokeza kuhesabiwa.
Akizitaja faida za kuendelea kuandika habari za Sensa Soko, amesema itawasaidia wananchi kupata uelewa wakutosha na kufahamu mafanikio mbalimbali yaliyopatikana hali itakayosaidia kushiriki kikamilifu kwenye Sensa nyingine,upatikanaji wa huduma za kijamii kutokana na Serikali kupeleka mipango ya maendeleo kulingana na idadi ya watu walioongezeka.
Akizungumza mara baada ya kupatiwa mafunzo hayo mwandishi wa habari wa Gazeti la Tanzania Daima Clara Matimo, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kupanua wigo wa muendelezo wa habari za Sensa kwa manuufaa ya Taifa kwani waandishi wengi huwa hawaandiki mambo mbalimbali ambayo jamii inatamani kujua ikiwemo mabadiliko ya huduma za kijamii zilizotolewa baada ya Sensa.
Aidha Matimo ameipongeza OJADACT kwa kutoa mafunzo hayo muhimu katika tasnia ya habari, huku akiiomba Serikali kuwa na utaratibu wa kuaanda mafunzo kama hayo kwa waandishi wa habari kwa kuwa na kundi muhimu katika kuwaelimisha Wananchi umuhimu wa kushiriki kwa ukamilifu zoezi la sensa.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,amesema vyombo vya habari vimesaidia sana kupeleka taarifa ya umuhimu wa Sensa kwenye Jamii, huku akiwataka waandishi wa habari kutumia mafunzo hayo kama nyenzo muhimu katika kuendelea kuihabarisha jamii umuhimu wakuhesabiwa kabla na baada ya zoezi la Sensa kukamilika.