******************************
Na Kassim Nyaki-NCAA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo tarehe 19 Agosti, 2022 amewaaga wananchi wanaohama kutoka Ngorongoro kwenda kijiji cha Msomera Wilayani Handeni ambayo ni awamu ya pili kundi la Kwanza.
Mhe. Majaliwa ameendelea kuwapongeza wananchi hao kwa uamuzi wa kujiandikisha kwa hiari na kuamua kupisha shughuli za Uhifadhi na kuhamia Msomera ambako Serikali imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 4000 lililowekewa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii kwa ajili ya wananchi hao.
Ameongeza kuwa katika kijiji cha Msomera wananchi hao watapata fursa ya kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara, kupewa nyumba yenye hati na eneo la ekari 2.5 pamoja na ekari 5 za kulima na huduma zingine za kijamii kama afya, shule, umeme, maji, mawasiliano, majosho na malisho bora ambapo walipokuwa Ngorongoro walikosa fursa hizo.
Amesisitiza wananchi hao kupuuza taarifa za upotoshaji zinazodanganya wananchi kuwa wanakoenda hakuna huduma na malisho ya mifugo yao.
“Serikali itaendelea kuwawekea miundombinu yote muhimu kuhakikisha kila kundi linaloenda linatumia fursa hiyo kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya maisha yao “alisema Waziri Mkuu huyo.
Katika tukio hilo Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa taasisi za kimataifa kutambua kuwa wananchi wanaoishi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wanajiandikisha kwa hiari yao wenyewe bila kushinikizwa na mtu na kazi ya serikali ni kuwaandalia wananchi hao mazingira rafiki na wezeshi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela amebainisha kuwa zoezi la uhamasishaji na uandikishaji unaendelea vizuri ambapo hadi kufikia tarehe 18 Agosti, 2022 jumla ya kaya 1,002 zenye jumla ya watu 5,382 zimejiandikisha kuhama kwa hiari na jumla ya Mifugo 13,717 imeshahamishiwa Kijiji cha Msomera na yote iko katika hali nzuri.
Katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NCAA Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo amewashukuru wananchi wa Ngorongoro kwa ushirikiano wanaoipa Serikali katika zoezi hilo na kuwaomba wampokee kama mwanangongoro ili kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.
Zoezi la kuhamisha wakazi walio tayari kuhamia Msomera ulianza tarehe 16 Juni, 2022 ambapo utaratibu wa kuhamisha wananchi hao ulizingatia ushirikishwaji wa wananchi na kuzingatia haki za binadamu.