Picha mbalimbali za Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kibaha..(Picha zote na Mwamvua Mwinyi)
…………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
HALMASHAURI ya wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani imepania kuendelea kukaa kileleni katika ukusanyaji wa mapato nchini ,kwa kuimarisha makusanyo ya ushuru wa mauzo ya viwanja eneo la kimkakati la Kwala pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwenye vyanzo mbalimbali.
Aidha ,imejipanga kuwachukulia hatua za kisheria wale watakaobainika kusababisha upotevu wa fedha na kukwepa kulipa ushuru.
Akielezea mkakati huo ,wakati wa Baraza la madiwani ,Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha ,Arasto Mpangala Makala alieleza, kipindi cha nyuma hawakufanya vizuri Ila wanashukuru kwa ushirikiano,ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa mapato umesaidia Halmashauri sasa imekuwa ya kwanza Kitaifa kwa kukusanya asilimia 247 ya makisio yake ya mwaka.
Alisema ,kwa mafanikio hayo watabana mianya ya upotevu wa makusanyo ,wataongeza kasi ya uimarishaji vyanzo vya mapato na kubuni vyanzo vipya ili kuongeza mapato 2022-2023.
Hata hivyo, Makala alifafanua hadi kufikia June 30 mwaka huu walikusanya Bilioni 28.6 sawa na asilimia 68 ya lengo kati ya fedha hizo walikuwa na Bilioni 3.8 ambazo ni mapato ya ndani ya vyanzo vya masharti na visivyo vya masharti.
Alitaja chanzo kikuu kinachowaongezea mapato ni ushuru wa mauzo ya viwanja eneo la kimkakati Kwala,ambalo walikusanya Bilioni 2.5 sawa na asilimia 124 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24 ,chanzo kingine ni ada na faini , mifugo na ukaguzi wa nyama .
“Mkakati wetu ni kuendelea kubaki kileleni hivyo tunaimarisha eneo la Kwala ambalo ni la kibiashara,lipo vizuri kwani kuna eneo la viwanda 300 vitakavyojengwa chini ya Kampuni ya SINOPAN ambapo heka 1,500 zimetengwa ,hatua iliyopo sasa ni kuandaa michoro na vijiji 16 vinavyozunguka eneo hilo vitatangazwa kuingizwa kwenye mpango kutoka sheria ya ardhi namba 5 kwenda namba 4 kwa mujibu wa sheria”alibainisha Makala.
Arasto Makala aliongeza kueleza ,eneo hilo linapangwa Kuwa la kisasa ,mpango mwingine uliopo ni kwamba mabasi ya mwendo Kasi yatafika, malori na makontena badala ya kushushwa Dar es Salaam itakuwa Kwala Bandari Kavu na DAWASA inapeleka maji ili kuondoa changamoto ya maji .
Nae Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Pwani,Hawa Mchafu aliitaka Halmashauri hiyo kusimamia miradi ya maendeleo na kuhakikisha inamalizika kwa wakati .
“Wakati tukisifika kwa ukusanyaji wa mapato , Halmashauri ionekanane ikiwa na miradi ya maendeleo ,fedha zifike kwa wakati kwenye miradi ili isibaki viporo”Licha ya hili ,nawapongeza kwa usimamizi mzuri wa kukusanya mapato”alisisitiza Mchafu.
Akichangia hoja, diwani na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira alisema ,nafasi ya kwanza wameipata kutokana na kwenda na Kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuwajibika .
Alieleza, kipindi cha nyuma hawakufanya vyema ,wakatafiti na kubaini tatizo ni ufuatiliaji haba ,wakaunda timu ya ufuatiliaji mapato na hatimae wameona matunda yake.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ,Josephina Gunda alielezea kwamba ,chanzo Cha stendi ,mkaa,minada na mchanga haikufanya vizuri ,kwasasa wamejielekeza kufanya ufuatiliaji na kubadilisha mfumo wa ukataji ushuru kwa kuwabana wakata ushuru ambao sio waaminifu.