Mkurugenziwa Redleaf Studio, Augustino Athanas maarufu kwa jina la AsheryWilz akizungumza wakati wa uzinduzi wa studio za kisasaza Redleaf mkoani Iringa
Mkurugenziwa Redleaf Studio, Augustino Athanas maarufu kwa jina la AsheryWilz kulia akiwa na meya wa manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada wakati wa uzinduzi wa studio za kisasa za Redleaf
Meya wa manispaa ya Iringa akifurahia na mkurugenzi wa Redleaf Studio, Augustino Athanas maarufu kwa jina la AsheryWilz wakati wa uzinduzi wa studio hizo
Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Lony Bway na Shedy wakitumbuiza wakati wa uzinduzi wa studio hizo (Picha zote na Denis Mlowe)
……………………………….
NA DENIS MLOWE, IRINGA
MEYA wa manispaa ya Iringa, Ibrahimu Ngwada amezindua studio ya kisasa ya muziki iliyoko mkoani Iringa iliyochini ya kampuni ya Redleaf Intertainment chini ya mkurugenzi wake Augustino Athanas Ashery’s.
Uzinduzi wa studio hizo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya burudani huku mgeni rasmi akiwa Mstahiki Meya Ibrahim Ngwada akisindikizwa na madiwani mbalimbali na diwani mwenyeji na baadhi ya wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa wakiongozwa na Lony Bway ambaye yuko chini ya studio hizo.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Meya Ngwada alisema studio hiyo itakuwa mkombozi kwa wasanii wengi wa Nyanda za Juu Kusini ambao walikuwa wakifanya kazi zao nje ya ya mkoawa Iringa kwa lengo la kupata ubora zaidi wa nyimbo zao na amedai kuwa uwepo wa studio hiyo utawasaidia wasanii kuwa na kazi zenye ubora wa kimataifa kutoka mkoani Iringa
Ngwada alisema kuwa wasanii wengi wamekuwa wakiamini kwamba studio bora ziko jijini Dar es Salaam pekee lakini kwa uwekezaji huu utasabisha wasanii wengi waweze kuja mkoani hapa na kuweza kurekodi nyimbo zao na kupata ubora mkubwa utakaowezesha nyimbo mbalimbali kufika ngazi za kimataifa.
Alisema kuwa hakika studio za Redleaf zitakuwa mkombozi kwa tasnia ya burudani ya nyanda za Juu Kusini kwani kasumba imejengeka kwamba bila kufanya kazi nje ya Iringa basi hakuna ubora hivyo studio hizi zitapandisha hadhi mkoa wa Iringa na kuufanya muziki wake hadhi ya kimataifa ambayo wasanii wamekuwa wakiitafuta kwa miaka mingi hususani kutoka mkoani Iringa na kuifanya kuwa kubwa zaidi kisanaa.
Alimpongeza mkurugenzi wa Redleaf Intertainment Ashery kwa kuweza kuwekeza studio za kisasa mkoani Iringa hali ambayo ni mfano wa kuigwa kwa wadau mbalimbali katika kukuza sekta ya muziki wa kizazi kipya na muziki mwingine na kutoa wito kwa wafanyabiashara na makampuni kuja kuwekeza mkoani hapa
.
Aliongeza kwa kuwataka vijana na viongozi mbalimbali waliokuwepo katika uzinduzi huo kuhakikisha pia wanaunga juhudi za serikali ya awamu ya tano kwa kujitokeza kuhesabiwa sensa ili serikali iweze kuweka mipango ya maendeleo vyema kwa kutambua idadi kamili ya wananchi wake.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenziwa Redleaf Studio, Augustino Athanas maarufu kwa jina la AsheryWilz ambaye pia ni msaniiwa bongo fleva alisema kuwa licha ya kuzalisha muziki studio hizo zitafanya matangazo mbalimbali ya kibiashara kutoka katika makampuni, radio mbalimbali na watu binafsi ,kuandaa matamasha mbalimbali kama fasheni show, nashughuli zote zinazohusisha burudani.
Alisema kuwa katika studio hizo wamewasaini wasanii wanne ambao watakafanya kazi zao hapo ambao wako ndani ya mkataba wakiongozwa na mkurugenzi mwenyewe AsheryWilz na kuweza kufanya kazi na wasanii wengine kama Sheby Medicine, Belle 9, Bright na Ibra Nation.
Ashery Wilz alisema kuwa wamejipanga vyema kuleta ushindani wa soko la muziki wa kizazi kipya ambao kwa sasa ni biashara kubwa nchini kwa kuwa nawazalishaji mahiri ambao wana umakini wa hali ya juu katika kazi chini ya mzalishaji Frodolassna Ben Zuzu.
“Huu ni uwekezaji mkubwa ambao nimefanya na natarajia kwa kiasi kikubwa kufanya kazi na wasanii mbalimbali ambao watafika hapa ndani ya himaya hii,” alisema
Kwa kuanza wameanza na kutoa EP yenye jina la Honest ikibebwa na nyimbo 7 ambapo wasanii mbalimbali wameshiriki katika nyimbo zilizoko na zinazobeba studio hizo na kusikilizwa kwa mara ya kwanza kwenye uzinduzi huo ambapo wasanii walioko kwenye Ep hiyo ni Ashery Wilz, Ibra Nation na Lony Bway na kutoa wito kwa wapenda burudani kuisikiliza kwenye mitando yote ya muziki.