Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa usalama wa chakula katika ukanda mzima wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzisihi nchi hizo kuwekeza kwenye ‘Uchumi wa Buluu’.
Rais Samia amependekeza hayo katika Mkutano wa 42 wa SADC uliofanyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumzia uwiano wa kijinsia waliokubaliana katika ukanda huo, Rais Samia amesema Tanzania imejitahidi kutoa fursa kwa wanawake hasa katika nafasi za uongozi za kimkakati.
Miongoni mwa nafasi hizo za uongozi serikalini na bungeni ni pamoja na za uwaziri wa Ulinzi, Mambo ya Nje, Uwekezaji, Utalii pamoja na nafasi ya Spika wa Bunge.
Rais Samia alitoa maoni yake kwa lugha ya Kiswahili ikiwa ni jitihada za kuchapusha matumizi ya lugha hiyo miongoni mwa nchi za SADC.
Katika mkutano huo uliopitisha maazimio 27 Rais Samia amesisitiza uharakishwaji wa mchakato wa Kiswahili kupitishwa rasmi kama lugha ya nne ya Jumuiya ya SADC.
Mkutano huo wa SADC pia ulishuhudia makabidhiano ya Uenyekiti kutoka kwa Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera na sasa nafasi hiyo imechukuliwa na Rais wa DRC, Felix Tshisekedi.
Rais Samia leo atafanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini DRC ambapo pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Felix Tshisekedi.