Nahodha wa meli ya MV Liemba Titus Benjamin (kushoto) akimueleza historia ya meli ya MV Liemba kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MSCL Meja. Jenerali. Mst. John Mbungo (mwenye suti ya Bluu) wakati alipofika kutembelea na kukagua meli za MSCL zilizopo Mkoani Kigoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi MSCL Meja. Jenerali. Mst. John Mbungo akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya MSC na watumishi wa MSCL tawi la Kigoma.
Meli ya MV Liemba
………………………………………
Na. Abdulrahman Salim – MSCL
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL)Meja Jenerali Mst. John Mbungo amempongeza Rais wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Shilingi Bilioni 45.1 kwa ajili ya kujenga meli mpya pamoja na kuzikarabati meli zilizokuwa hazitoi huduma kwa wananchi katika ziwa Tanganyika.
Pongezi hizo amezitoa tarehe 17.08.2022 baada ya kukagua mradi wa ukarabati wa meli ya kubeba mafuta ya MT Sangara pamoja na kuzitembelea meli ya MV Mwongozo na meli kongwe ya MV Liemba zilizopo katika bandari ya Kigoma, mkoani Kigoma.
“Kwakweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutoa fedha nyingi sana katika miradi hii na kuhakikisha kwamba meli zetu zinakarabatiwa, mbeli ambazo zinahitaji kutoa huduma ndani ya maji haya ya maziwa makuu, zifanye kazi na kuwafikia majirani,” Alisema.
Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, ndg Philemon Bagambilana alisema kuwa, mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ya Awamu ya Sita imetenga shilingi bilioni 113 kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi wa meli huku Shilingi Bilioni 45.1 zitatekeleza miradi mitano katika Ziwa Tanganyika.
“Katika fedha hizo miradi mitano itatekelezwa Ziwa Tanganyika ikiwemo ujenzi wa chelezo cha kujengea meli maana kilichopo ni kikongwe na ndio kilichotumika kujengea MV Liemba ambacho kina zaidi ya miaka 100, sasa hizi meli kubwa zinazokuja kujengwa, hii miundombinu haiwezi ‘ku-support’ (kuhimili), kwahiyo serikali katika mwaka huu wa fedha itajenga chelezo kipya,”Alielezea.
Akitoa mchanganuo wa fedha hizo Meneja Tawi la MSCL Mkoani Kigoma ndg. Allen Butembero alisema kuwa meliya MV Liemba imetengewa shilingi bilioni 8.1, Ujenzi wa meli mpya ya mizigo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 3,000 imetengewa shilingi bilioni 12, na Ujenzi wa meli mpya ya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo imetengewa shilingi bilioni 12.
“Tunatarajia miradi hii ikikamilika itaweza kufufua tawi hili la Kigoma pamoja na kuleta tija kwa wananchi waishio katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kwani itapunguza gharama za usafirishaji wa abiria na mizigo.”